Michezo

AC Milan pia yamezea mate Victor Wanyama

January 10th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

AC Milan ni klabu ya hivi punde kuhusishwa na kiungo Victor Wanyama katika kipindi kifupi cha uhamisho cha Januari 1-31, 2020.

Taarifa nchini Uingereza zinasema kuwa mabingwa hao wa mataji 18 ya Ligi Kuu ya Italia wanataka wachezaji wa Tottenham Hotspur Wanyama na beki kutoka Argentina Juan Foyth ndiposa wamwachilie mshambuliaji wao Krzysztof Piatek ajiunge na klabu hiyo kutoka jijini London.

Inasemekana kocha Jose Mourinho anatafuta mshambuliaji huyo kutoka Poland wakati huu Spurs haina mfumaji wake hodari Harry Kane anayeuguza jeraha hadi mwezi Aprili.

Ripoti zinadai kuwa Milan imekataa ofa ya kwanza ya Spurs ya kutaka kuchukua Piatek kwa mkopo mwezi huu kabla ya kununua kabisa mwisho wa msimu.

Milan inasemekana imekataa mambo ya Piatek kuchukuliwa kwa mkopo na kuwa itaridhika kubadilishana Piatek na wachezaji Wanyama na Foyth.

Mbali na Milan, Wanyama pia amehusishwa na Galatasaray (Uturuki), Hertha Berlin (Ujerumani), Norwich na West Ham (Uingereza), Celtic (Scotland) na klabu kutoka China.

Aidha, taarifa nchini Uturuki zilidai mapema juma hili kuwa Wanyama atasaini kandarasi ya mwaka mmoja na nusu na miamba Galatasaray mnamo Januari 10, 2020.