AC Milan watoka sare dhidi ya Cagliari kwenye Serie A

AC Milan watoka sare dhidi ya Cagliari kwenye Serie A

Na MASHIRIKA

AC Milan walishindwa kuwapepeta Cagliari katika Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo Jumapili na hivyo kuwapa Juventus matumaini tele ya kukamilisha kampeni za msimu huu ndani ya orodha ya nne-bora na hivyo kujikatia tiketi ya kunogesha soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) muhula ujao.

Chini ya kocha Stefano Pioli, AC Milan kwa sasa wanashikilia nafasi ya nne jedwalini kwa alama 76 sawa na nambari tatu Napoli waliowapepeta Fiorentina 2-0 katika gozi jingine la Jumapili.

Masogora wa Pioli walishindwa kujiamini dhidi ya Cagliari waliowalazimishia sare tasa. Ilikuwa mara ya kwanza tangu 1999 kwa Cagliari kuokota alama dhidi ya AC Milan kwenye mchuano wa Serie A ugenini.

Juventus wanaotiwa makali na kocha Andrea Pirlo wanakamata nafasi ya tano kwa alama 75. Ina maana kwamba ushindi kwa Napoli na AC Milan kwenye michuano yao ya mwisho msimu huu utawanyima Juventus fursa ya kushiriki soka ya UEFA muhula ujao wa 2021-22. Itakuwa mara ya kwanza kwa kikosi hicho kuwa nje ya mashindano hayo ya haiba kubwa barani Ulaya tangu 2011-12.

Hata hivyo, matumaini finyu ya Juventus yanategemezwa kwa matokeo ya gozi gumu litakalowakutanisha AC Milan na Atalanta ambao tayari wana uhakika wa kukamilisha kampeni za muhula huu ndani ya mduara wa nne-bora.

Iwapo AC Milan watakomolewa nao Verona wawachape Verona, basi Juventus watamaliza msimu ndani ya nne-bora iwapo watawapepeta Bologna katika mchuano wao wa mwisho wa msimu huu.

Juventus waliwakung’uta mabingwa wapya wa Serie A, Inter Milan, kwa kichapo cha 3-2 mnamo Jumamosi. Kocha wa zamani wa Chelsea, Antonio Conte, ndiye aliongoza Inter Milan kukomesha ukiritimba wa Juventus kwenye soka ya Serie A. Juventus walikuwa wakiwania taji la Serie A kwa mara ya 10 mfululizo muhula huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO 

You can share this post!

Mshindi wa Ligue 1 msimu huu kujulikana siku ya mwisho ya...

UDAKU: Dele Alli si mchache! Ameingiza boksi binti wa kocha...