Acakoro Ladies yanyeshea St Annes Eaglets 5-1

Acakoro Ladies yanyeshea St Annes Eaglets 5-1

Na JOHN KIMWERE

MCHANA nyavu, Catherine Omondi alicheka na wavu mara mbili na kusaidia Acakoro Ladies kushinda St Annes Eaglets mabao 5-1 kwenye nusu fainali ya Mkoa wa Nairobi kuwania taji la Chapa Dimba na Safaricom, Season Three.
Acakoro ilijikatia tikiti ya fainali na kujiongezea tumaini la kuhifadhi ubingwa wa taji hilo katika mkoa wa Nairobi na kushiriki fainali za kitaifa kwa mara ya pili mfululizo.
Kwenye nusu fainali hizo zilizopigiwa uwanja wa Jamhuri High, wasichana wa Beijing Raiders walikomoa Kibagare Girls mabao 3-0.
”Nilikuwa nafahamu kuwa mechi hiyo ingekuwa ngumu nashukuru wasichana wangu kwa kujikatia tikiti ya fainali,” alisema kocha wa Beijing Raiders, Mark Okwiri.
Kwenye nusu fainali za wavulana, Dagoretti Mixed na Hakati Sportiff kila moja ilisajili ushindi wa mabao 3-0 dhidi ya KSG Ogopa na Brookshine Academy mtawalia.
Verine Acheing wa St Annes Eaglets akiwa na mpira baada ya kumchenga Florence Achieng wa Acakoro Ladies kwenye nusu fainali ya wasichana Mkoani Nairobi kuwania taji la Chapa Dimba na Safaricom Seasom three, katika uwanja wa Jamhuri High Nairobi. Acakoro ilishinda mabao 5-1. Picha/ John Kimwere
Wachezaji wa Acakoro walianza mchezo huo kwa kasi ambapo Catherine Omondi alifunga bao la kwanza dakika ya pili kabla ya Florence Achieng na Sylvia Makungu kuongeza bao moja kila mmoja dakika ya 14 na 17.
Kisha ndani ya kipindi cha pili, Diana Hashina alifunga bao la nne naye Catherine akiongoza bao lake la pili.
Shantel Muthoni aliifungia St Annes Eaglets bao la kufuta machozi.
Naye Maximila Robi alitingia Beijing Raiders mabao mawili huku Martha Mutheu akitikisa nyavu mara moja. Kwa upande wa Hakati, Lewis Bandi, Juma Otieno na Lewis Mutava kila mmoja aliifungia bao moja.
Katika fainali Acakoro Ladies ilipangwa kucheza na Beijing Raiders nao wavulana wa  Dagoretti Mixed waliratibiwa kucheza dhidi ya Hakati Sportiff kutafuta bingwa wa mkoa wa Nairobi.
Mabingwa wa taji hilo, kitengo cha wavulana na wasichana watajikatia tiketi ya kushiriki fainali za kitaifa ambazo zimepangwa kuandaliwa mjini Mombasa Mwezi Juni mwaka huu.
Mchezaji wa Dagoretti Mixed, Alex Munga (katikati) akijaribu kupitia katikati ya mabeki wa KSG Ogopa FC kwenye nusu fainali ya wavulana ya mkoa wa Nairobi kuwania taji la Chapa Dimba na Safaricom Seasom three, katika uwanja wa Jamhuri High Nairobi. Dagoretti ilishinda mabao 3-0. Picha/ John Kimwere
Kando na hayo, timu hizo mbili kila moja itapokea kitita cha Sh200,000. Nazo timu zitakaomaliza katika nafasi mbili kila moja itapongezwa kwa Sh100,000.
Washindi wa eneo hilo watajiunga na wenzao kutoka maeneo mengine kufuzu kwa fainali za kitaifa. Wavulana watajiunga na wenzao wa Berlin FC ya Garissa Mkoa wa Kaskazini Mashariki, Ulinzi Youth ya Mkoa wa Kati , Tumaini school (Mkoa wa Mashariki) na Yanga FC kutoka Malindi Mkoa wa Mombasa.
Wasichana watajiunga na Falling Waters kutoka Mkoa wa Kati, Isiolo Starlets (Mkoa wa Mashariki) na Kwale Ladies malkia wa taji hilo katika Mkoa wa Mombasa.

You can share this post!

Raila anyakua kazi ya Ruto

ANN NJOROGE: Filamu Kenya ina malipo duni lakini usife moyo

adminleo