Michezo

Acakoro Ladies yatinga fainali Chapa Dimba, South B United yanoa

June 24th, 2019 2 min read

Na JOHN KIMWERE

MATUMAINI ya wavulana wa South B United kubeba ubingwa wa kitaifa wa taji la Chapa Dimba na Safaricom Season Two, yaligonga mwamba ilipobamizwa kwa mabao 3-2 na Al-Ahly kupitia mipigo ya matuta kwenye nusu fainali ya iliyopigiwa Kinoru Stadium Meru.

Nao wachana nyavu wa Manyatta United walijikatia tikiti ya fainali baada ya kuandikisha ushindi wa mabao 2-1 mbele ya Lugari Blue Saints.

Kitengo cha wasichana, wawakilishi wa Mkoa wa Nairobi, Acakoro Ladies ilinyanyua Changamwe Ladies mabao 4-2 na kusonga mbele, huku Kitale Queens ikizaba Barcelona Ladies ya mabao 6-1 na kufuzu kwa fainali.

Wavulana wa Manyatta United wawakilishi wa Mkoa wa Nyanza waliopigiwa upatu kutwaa taji hilo kabla ya fainali hizo walivuna ufanisi huo kupitia Peter Ochieng na Ibrahim Ochieng waliotinga bao moja kila mmoja. Naye Allan Musonye alifungia Lugari Blue Saints ya Mkoa wa Mkoa wa Magharibi bao la kufuta machozi.

”Kusema ukweli kushinda mechi yetu haikuwa mteremko maana wapinzani wetu walishusha ushindani mkali kweli kweli,” mchezaji wa Manyatta United Ibrahim Ochieng alisema na kuongeza kuwa wanajipanga kukabili shughuli nzito dhidi ya Al-Ahly katika fainali.

Al-Ahly iliishinda South B United kwa mikwanju ya penalti baada ya kutoka nguvu sawa mabao 2-2 katika muda wa kawaida. Mabao ya Al-Ahly yalifumwa na Abdirahim Abdullahi na Marion Idd nayo Wilson Anguli na Kepha Wanjala walitingia South B United.

Licha ya South B United kukosa tikiti ya fainali kocha wake, John Mandela alishukuru wachezaji wa kikosi chake kwa kujituma kisabuni kwenye mchezo huo. Katika fainali ya wavulana, Manyatta United iliratibiwa kukwaruzana na Al-Ahly FC ya Mkoa wa Bonde la ufa.

Baada ya wavulana wa Mkoa wa Nairobi kubanduliwa matumaini ya Nairobi kubeba taji hilo yalibakia kwa wasichana wa Acakoro Ladies. Acakoro Ladies ilionyesha mchezo safi kwenye nusu fainali na kunasa tikiti ya kushiriki fainali kupitia Catherine Awuor aliyepiga ‘Hat trick’ huku Sylvia Makhungu akitikisa wavu mara moja.

Nayo Changamwe Ladies ilipata mabao ya kufuta machozi kupitia juhudi zake Saumu Kahindi na Nancy Akinyi walicheka na wavu mara moja kila mmoja.

Kitale Queens ilionyesha kazi nzito mbele ya Barcelona Ladies ya Mkoa wa Kati ambapo ilibeba tikiti ya fainali kupitia juhudi zao Peris Nafula na Agneta Marondo waliopiga mbili safi kila mmoja nao Metrine Nanjala na Daisy Busia kila mmoja alicheka na wavu mara moja.

Bao la kufuta machozi la Barcelona Ladies lilitingwa na Jane Njeri aliye mfungaji hodari wa kikosi. Fainali ya warembo iliratibiwa kushirikisha Acakoro Ladies na Kitale Queens. Mshindi wa taji hilo la kitaifa kwa wavulana na wasichana kila mmoja atatuzwa kitita cha Sh1 milioni.