Makala

Acha kukaa vibarazani, jipe shughuli – Ushauri

March 26th, 2024 2 min read

NA BENSON MATHEKA

KANDO na taaluma ambayo watu husomea, kuna kazi nyingi ambazo watu wanaweza kufanya na kujiendeleza kimaisha badala ya kusubiri miujiza au kujihusisha na vitendo vya ukiukaji sheria, wataalamu wa ajira na wanauchumi wanasema.

Badala ya mtu kupoteza muda akisubiri kazi aliyosomea hadi akahitimu ipatikane, watalaamu wanasema ni muhimu kujaribu mambo mengine.

“Ushauri wangu ni kuwa ikiwa kazi hazipatikani, mtu hafai kukaa kitako akisubiri au akiendelea kutafuta kazi aliyosomea au kuhusika na vitendo vilivyo kinyume na sheria. Anaweza kujaribu mambo tofauti na agundue uwezo wake mwingine,” asema Bw Simon Kavisi, mtaalamu wa ajira.

Anasema kuna watu waliofuata ushauri huu na wamefanikiwa pakubwa maishani.

“Ukweli ambao watu wanapasa kubaini ni kwamba maisha hayasimami kuwasubiri hadi wapate kazi walizosomea na kuhusika na uhalifu ni kujitia mashakani. Maisha huwa yanaendelea na nguvu kuendelea kupungua katika mili yao. Wanaweza kutumia nguvu zao kujaribu mambo mengine ya kujipatia riziki,” asema Bw Kavisi.

Mtaalamu huyu anakumbusha vijana kwamba wanaweza kujifunza mambo mengi kupitia mitandao.

“Tofauti na enzi za zamani ziku hizi kuna mtandao ambao mtu anaweza kupata maelezo na habari muhimu kuhusu kazi anayochagua kufanya. Nafikiri ni uvivu unaofanya watu kukosa kujaribu mambo mapya,” asema Kavisi.

Kulingana na Bw Derrick Wekesa, mshauri wa masuala ya ajira jijini Nairobi wanachokosa watu wengi ni mwongozo wa wanavyoweza kukabiliana na ukosefu wa ajira.

“Kuna watu ambao hawapati ushauri mpana kuhusu ajira. Wanachofanya ni kusomea kozi wanayochaguliwa kusomea vyuo vikuu. Kuna haja ya walimu na wazazi kuwaeleza wanafunzi ukweli wa mambo. Kwamba mtu anaweza kufanya kazi tofauti na aliyosomea chuo kikuu na imfanye afaulu sana maishani,” asema.

Anasema kukataa kitako kusubiri kazi ipatikane ni kuharibu wakati na kushiriki uhalifu ni kuweka maisha hatarini na hakuna manufaa yoyote kwa mhusika.

“Jaribu mambo mengine kwa sababu kukaa kitako na kuomboleza kwa kutopata kazi uliyosomea au unayopenda hakutakusaidia. Mtu huwa anatayarisha maisha yake wakati ana nguvu na wasemavyo wahenga, ujana ni kama moshi, ukienda haurudi,” ashauri.

Kuhusu uhalifu, Bw Wekesa ana mengi ya hekima kuwafaa wanajamii.

“Ni hatari na mapato ya uhalifu hayana baraka. Ni laana na busara ni kuepuka vitendo vinavyokusesha amani. Kuna mambo mengi ya kufanya na kuleta mapato,” asema Bw Wekesa.

Bw Kavisi anakubaliana naye na kuongeza kuwa wakufunzi wanapasa kufunza wanafunzi wao kuwa wabunifu. Kuhusu mtandao, wataalamu wanasema kuna haja ya vijana kuhamasishwa jinsi ya kuutumia kujijenga kimaisha ili wasitumbikie katika uhalifu wa mtandao

“Kuna mambo mengi katika mtandao ambayo watu wanatumia kujipatia mapato na kwa sababu sio vijana wote wanaojua kuutumia hasa sehemu za mashambani, juhudi zinapasa kufanywa kuwahamasisha waweze kunufaika na  huduma hizo,” asema Bw Kavisi.