Achani afokea wanaompinga ugavana Kwale

Achani afokea wanaompinga ugavana Kwale

NA SIAGO CECE

GAVANA mteule wa kaunti ya Kwale, Fatuma Achani, amewafokea wapinzani wake wanaodai kulikuwa na dosari za uchaguzi katika kaunti hiyo, huku akiwataka kutafuta suluhu ya kisheria kutoka kwa mahakama badala ya kumharibia jina.

Bi Achani anashikilia kuwa alishinda kwa haki, na akawataka wanaosema kuwa walinyimwa ushindi wao wanapaswa kukusanya ushahidi na kuelekea mahakamani kupinga ushindi wake.

“Nilishinda kwa haki. Ukiangalia kura zote utaona nilipata kura nyingi katika maeneobunge yote na huo ni uthibitisho tosha kwamba nilistahili kushinda,” Bi Achani alisema.

Alikuwa akizungumza huko Tiwi Magodzoni, kaunti ndogo ya Matuga ambapo alikuwa anasherehekea ushindi wake na wakazi.

Bi Achani, ambaye ameandika historia kwa kuchaguliwa mwanamkwe gavana wa kwanza eneo la Pwani, alidai alikuwa anatishiwa na wale aliowashinda katika uchaguzi ambao walizua mvutano katika kaunti hiyo kwa madai yao ambayo yanawachochea vijana.

“Kama gavana wa pili wa kaunti hii, niko tayari kukabiliana nao na tayari kwa matokeo yoyote. Watatu hao wanapaswa kufuata sheria ikiwa wanatatizwa na wakome kusababisha uhasama miongoni mwa wakazi,” akasema.

Matamshi yake yanajiri baada ya wawaniaji watatu walioshindwa kinyang’anyiro cha ugavana kuibua wasiwasi kuhusu uchaguzi wa Kwale wakidai kulikuwa na kasoro nyingi na dosari ambazo walikuwa na ushahidi.

Mwishoni mwa juma, Lung’anzi Chai, Prof Hamadi Boga na Chirau Ali Mwakere walipinga ushindi wa Bi Achani wakisema hawakuridhishwa na michakato ya IEBC.

Watatu hao kwa pamoja walisema wataelekea mahakamani kutafuta haki.

Prof Boga alisema hana imani katika kutaja kasoro mbalimbali zinazozua maswali kuhusu matokeo ya uchaguzi huo.

Haya yanajiri huku viongozi waliochaguliwa Kwale wakiahidi kufanya kazi kwa usawa ili kuhakikisha kuwa wakazi wanapata huduma zinazohitajika.

Akizungumza huko Matuga, seneta mteule wa Kwale Issa Boy aliwaambia wapinzani wake kwamba wanapaswa kusahau yaliyopita na kuzingatia dhamira yao kuu ambayo ni utoaji wa huduma.

“Ninajua kwamba tumepigana sana wakati wa kampeni na huenda tumetupiana maneno ya chuki. Lakini ushindi wetu unamaanisha watu wetu wametuchagua hivyo tushirikiane kwa niaba yao,” alisema.

Kwa upande wake mwakilishi wa wanawake wa Kwale Fatuma Masito aliyechaguliwa kwa tikiti ya ODM alisema yuko tayari kufanya kazi na kiongozi huyo mwingine aliyechaguliwa.

“Ni wakati wa kuweka tofauti zetu nyuma yetu na kuhakikisha kuwa tumeungana ili wakazi wote wa Kwale wapate,” alisema.

Kampeni za Kwale zilipamba moto wakati viongozi walipogawanyika kuhusu tofauti za vyama na kabila.

  • Tags

You can share this post!

Siraj apigana kuhakikisha amevalia jezi ya Harambee Stars

Chebukati asimulia mahangaiko yake, maafisa wa IEBC

T L