Achani arai wanawake wajitokeze zaidi kisiasa

Achani arai wanawake wajitokeze zaidi kisiasa

SIAGO CECE na KNA

NAIBU Gavana wa Kaunti ya Kwale, Bi Fatuma Achani, amerusha ndoano yake ya kisiasa kwa wanawake anapopanga kuwania ugavana mwaka ujao.

Huku akisisitiza kuwa ana uwezo wa kutosha kumrithi Gavana Salim Mvurya, atakayekamilisha hatamu yake ya uongozi 2022, alitoa wito kwa wanawake kuungana ili idadi yao iongezeke katika uongozi wa kisiasa.

Akizungumza jana wakati wa mkutano wa kustawisha wanawake kiuchumi, alisema idadi ya wanawake uongozini itaongezeka tu ikiwa watajitokeza kupigania nafasi hizo na kutetea uwepo wa uwakilishi mkubwa wa wanawake katika uongozi wa serikali.

“Kunafaa kuwe na idadi kubwa zaidi ya wanawake watakaotafuta nafasi za uongozi kama njia mojawapo ya kukabiliana na uhaba wao serikalini. Wakati Uchaguzi Mkuu wa 2022 unapokaribia, tunahitaji kuona wanawake wengi wakijitokeza kuwania nafasi za uongozi,” akasema.

Mkutano huo kwa jina ‘Wadada Pawa Forum’ katika Hoteli ya Mangro mjini Diani uliandaliwa na Baraza la Kitaifa la Makanisa Kenya (NCCK) kujadili nafasi zilizopo kwa wanawake uongozini.Kulingana na Bi Achani, changamoto ambazo hukumba wanawake katika siasa ni nyingi lakini wana uwezo kuzikabili iwapo watasaidiana.

Alitoa wito kwa wanawake kujisajili kama wapigakura na kisha wajitokeze kwa wingi kushiriki uchaguzi mkuu ujao, wala wasichukulie siasa kama jukumu la wanaume pekee.Kando na hayo, aliwahimiza wanawake wa Kaunti ya Kwale kushiriki katika biashara ili kujiendeleza kiuchumi.

Naibu Gavana aliwahimiza wanawake kuchukua mikopo inayotolewa na serikali ya kaunti ili kuanzisha biashara ndogo ndogo.Alisema kuwa, ili kufaidika na mikopo hiyo, wanawake wanafaa kuungana na kujisajili katika vikundi.“Kaunti imeweka kipaumbele mipango ya kuinua maisha ya wanawake na tungependa watumie nafasi hii maalum waliyopewa,” Bi Achani alieleza alipokutana na wanawake Ukunda.

Katika fedha hizo zinazotolewa na kaunti, wanawake, walemavu na vijana wanapewa mikopo inayotozwa riba ya chini ikilinganishwa na ile ya mashirika ya fedha.Vile vile, Bi Achani alisema kuwa ili sauti zao zisikike na wanufaike kikamilifu, wanawake wanapaswa kufuatilia habari kuhusu fursa walizotengewa katika serikali ya kaunti na kitaifa.

Isitoshe, aliwahimiza kushiriki katika vikao vya kujadili masuala ya umma, kama zile vya utengenezaji wa bajeti.Naibu kiongozi huyo wa kaunti alisema serikali za ugatuzi na ile ya kitaifa zimejitolea kuhakikisha kuwa makundi yaliyotengwa katika jamii; kama wanawake, vijana na walemavu, yanapata fursa ambazo zitawawezesha kuboresha maisha yao.

“Tumeweka hatua na sera kuhakikisha kuwa wanawake wa Kaunti ya Kwale wanafanikiwa katika nyanja zote za maisha,” alihoji. Akijipigia debe kuelekea Uchaguzi Mkuu 2022 hapo awali, Bi Achani alisema kuwa anataka kuendeleza miradi ya maendeleo aliyoanza katika kipindi chake kama naibu gavana.

Mradi wa kupeana pesa kwa vikundi ulianzishwa mnamo 2014. Katika mradi huo, serikali ya kaunti hutoa fedha kila mwaka kwa vikundi vya watu wanaotaka kuanzisha biashara. Hii ni katika mojawapo ya njia za kukuza uchumi wa kaunti hiyo.

You can share this post!

Karo: Magoha ataka watoto wafukuzwe

Kuhalalisha au kutohalisha bangi kutahitaji sera mwafaka