Siasa

Acheni siasa za pesa nane – Lonyangapuo

February 10th, 2024 2 min read

NA OSCAR KAKAI

ALIYEKUWA Gavana wa Kaunti ya Pokot Magharibi John Lonyangapuo amewasuta viongozi waliochaguliwa eneo la Kaskazini mwa Bonde la Ufa ambao wanaegemea Azimio la Umoja-One Kenya, kwa kufanya siasa za pesa nane na kusahau majukumu yao ya kutoa huduma kwa wapigakura.

Kulingana na Lonyangapuo, viongozi hao wa upinzani wanafaa kukubali kuwa walishindwa kwenye uchaguzi wa Agosti 9, 2022, na kukoma kuinyooshea kidole cha lawama serikali ya Kenya Kwanza.

Prof Lonyangapuo sasa anautaka muungano huo wa upinzani kukomesha siasa chafu na kumpa Rais William Ruto muda kutekeleza ahadi alizoahidi Wakenya wakati wa kampeni.

Kiongozi huyo ambaye aliasi mrengo wa Azimio na kujiunga na Kenya Kwanza punde tu baada ya uchaguzi mkuu, aliwataka wanasiasa kuwa na umoja na kukomesha siasa duni na badala yake kufanya siasa komavu.

“Tuitikie wito wa Rais Ruto wa kuiweka Kenya mbele kwanza kabla ya ubinafsi wetu,” alisema Prof Lonyangapuo.

Aliwatahadharisha wanasiasa dhidi ya kugawanya Wakenya kwa misingi ya kikabila, akiwakumbusha kuwa wakati wa siasa uliisha na Wakenya wanahitaji huduma.

“Kenya ni moja na Wakenya ni wamoja. Tuipe Kenya kipaumbele na watu wake,” alisema.

Akimpongeza Rais Ruto kwa uongozi wake wa ‘mfano bora’ na wa kukumbatia viongozi kutoka kwa upinzani, mtaalamu huyo wa hisabati aliwataka viongozi kwa ujumla kuacha chuki na kukumbatia uvumilivu kwenye siasa.

“Viongozi wa sasa wanafaa kushauriana na wale walioondoka .Usichukue mpinzani wako kama adui,” alishauri.

Aliwataka viongozi kukomesha tofauti zao za kisiasa na kufanya kazi pamoja licha ya mirengo yao ya kisiasa akisema kuwa umoja pekee utasaidia wao kupata maendeleo.

“Umoja ni nguzo ya uongozi na ili maendeleo kupatikana ni sharti viongozi waweke kando tofauti zao na kufanya bidii kutimiza ahadi na malengo,” akasema.

Prof Lonyangapuo aliwataka magavana wa sasa kutowafuta kazi maafisa ambao walikuwa na wapinzani wao.

Alisema kuwa kuna haja ya kuwa na nguvu ya pamoja kutoka kwa viongozi waliochaguliwa na wale ambao hawakuchaguliwa.

“Uchaguzi ulikwisha na sisi ambao tulishindwa tunafaa kuunga mkono wale ambao walifaulu. Wanafaa kupewa muda kutekeleza ahadi ambazo walitoa wakati wa kampeni. Tuwapatie muda waliochaguliwa wafanye kazi,” alisema.

Naye mbunge wa Kacheliba Titus Lotee (KUP) alisema kuwa yeye aligura muungano wa Azimio kwa kukosa ajenda.

Viongozi hao waliongea wakiwa eneo la Kanyarkwat.

[email protected]