MichezoSiasa

Echesa akodolea macho kutemwa kutokana na kiwango chake cha elimu

February 13th, 2018 1 min read

Bw Rashid Echesa aliyeteuliwa kusimamia Wizara ya Michezo. Picha/Maktaba

Na GEOFFREY ANENE

SAA chache kabla ya Bunge kuidhinisha majina ya Mawaziri waliohojiwa juma lililopita, ripoti zimeibuka kwamba Rashid Achesa Mohammed atatemwa.

Kwa mujibu wa tovuti ya Pulse Live, Achesa, ambaye aliteuliwa kuhudumu kama Waziri wa Michezo na Utamaduni, atatupwa nje ya orodha hiyo kutokana na kiwango chake cha chini cha masomo.

“Achesa aliacha kusoma katika darasa la saba,” tovuti hiyo limesema Jumatatu.

Limeongeza kwamba Kiongozi wa walio wengi bungeni, Aden Duale, ameitisha mkutano wa dharura wa wabunge wote wa chama cha Jubilee pamoja na Rais Uhuru Kenyatta kuunga mkono shughuli ya kumtema Achesa kutoka orodha hiyo.

“Achesa alishindwa kuelezea kinangaubaga kiwango chake cha elimu, lakini wasifu wake unaonesha aliacha shule akiwa katika darasa la saba,” tovuti hiyo ilisema ikinukuu idhaa ya Radio Citizen.

Achesa anafaa kujaza nafasi ya Dkt Hassan Wario, ambaye ameteuliwa kuwa Balozi wa Kenya nchini Austria.

Wanamichezo wengi hawakuridhika na Dkt Wario aliyehudumu kama Waziri wa Michezo, Utamaduni na Sanaa tangu mwaka 2013.