Habari Mseto

Achoma chakula cha msaada na kutoroka

August 10th, 2019 1 min read

Na SAMMY LUTTA

POLISI katika Kaunti ya Turkana wanamsaka mwanamume aliyeteketeza zaidi ya magunia 100 ya chakula cha msaada Ijumaa jioni.

Mkuu wa Kaunti Ndogo hiyo, Bi Esther Kiyonga, alisema mwanamume huyo aliwasha gurudumu la gari kijijini Nakoyo, Kaunti Ndogo ya Turkana Magharibi, mahali ambapo chakula hicho kilikuwa kinahifadhiwa.

“Chakula hicho kingefaidi waathiriwa wa njaa 1,100 na kilitarajiwa kupeanwa Jumamosi. Chakula kilichoteketezwa ni magunia 92 ya kilo 50 ya mahindi, magunia 18 ya kilo 50 ya maharagwe na mafuta ya kupikia,” Bi Kiyonga aliambia Taifa Jumapili.

Alieleza kuwa pindi mshukiwa huyo alipowasha moto, alitoroka kwa kuelekea kichakani.

Tukio hilo tayari limeripotiwa kwa kituo cha polisi cha Kakuma huku uchunguzi ukianzishwa ili kubaini sababu ya chakula hicho kuchomwa.

Wakazi waliombwa kuripoti kwa polisi watakapomwona jambazi hiyo.

Ilisemekana kuwa hivi maajuzi kumekuwa na mzozano kwenye mpaka hiyo wa Wadi ya Kalobeyei na Lopur jambo ambalo pia linachunguzwa kama kiini cha kisa hicho.

Laki sita

Serikali ya Kaunti ya Turkana mwezi Julai ilinunua chakula cha msaada cha kutosheleza watu zaidi ya 600,000 ambao wanaendelea kukumbwa na baa la njaa katika maeneobunge yote sita.

Miongoni mwa chakula ambacho kilinunuliwa ni magunia 107, 457 ya kilo 50 ya mahindi.

Baa la njaa katika kaunti hiyo lilisababishwa na ukosefu wa mvua na uvamizi wa nzige.

Mwanzoni mwa mwaka 2019, wanahabari walianzisha kampeni ya kuwachangia wakazi wa Turkana chakula.

Wahisani kadhaa, akiwemo Gavana wa Nairobi, Mike Sonko waliitikia mwito huo na kupeleka chakula.