Achoma nyumba ya mpangaji kwa kutolipa kodi ya Sh2,000

Achoma nyumba ya mpangaji kwa kutolipa kodi ya Sh2,000

Na KNA

POLISI wameanzisha msako dhidi ya mshukiwa aliyeteketeza nyumba ya mpangaji wake kwa kukosa kulipa kodi ya Sh2,000 kjijini Kalolenyi mjini Voi, Jumamosi jioni.

Maafisa wa polisi wameanzisha msako dhidi ya mshukiwa huyo ambaye ni mmiliki wa nyumba aliyoteketeza.

Kulingana na majirani, mmiliki huyo wa nyumba alianza kuvutana na mpangaji wake kuanzia Jumamosi asubuhi kuhusiana na kodi ya nyumba ya mwezi wa Juni.

Mpangaji, ambaye ni mchuuzi, alikuwa ameahidi kulipa nusu ya kodi na kisha kumalizia kiasi kilichosalia baadaye. Lakini mshukiwa alikataa katakata kupokea Sh1,000.

Baadaye, mshukiwa alirejea jioni akiwa amebeba petroli na kuteketeza nyumba hiyo. Mpangaji hakuwepo nyumbani wakati wa mkasa huo.

Mkuu wa Polisi wa Voi, Joseph Chesire alisema maafisa wa usalama wameanzisha uchunguzi na wanamsaka mshukiwa ili afunguliwe mashtaka ya uharibifu wa mali.

“Kuna mahakama ya kushughulikia mizozo ya kodi za nyumba na mmiliki wa nyumba hafai kujichukulia sheria mkononi kuteketeza mali ya wapangaji wake,” akasema.

You can share this post!

Magari ya Probox sasa yapigwa marufuku ya uchukuzi wa umma

Yabainika gari la seneta lililodaiwa kuibwa lilitwaliwa na...

adminleo