Achuma hela kwa kutia nakshi vinyago Mombasa

Achuma hela kwa kutia nakshi vinyago Mombasa

NA CHARLES ONGADI

CHANGAMWE, MOMBASA.

NI katika mojawapo ya karakana maarufu ya uchongaji vinyago eneo la Changamwe, Mombasa, ninakokutana na Mbithe Reuben.

Mama huyu mkakamavu mwenye umri wa miaka 38, anaonekana mtulivu na kuchangamkia mno kazi yake licha shughuli za kawaida za uchongaji vinyago zikizidi kupamba moto.

Ni mojawapo ya karakana iliyo maarufu eneo la Changawe kwa uchongaji vinyago vya wanyama kila sampuli na watu hasa kutoka jamii ya Maasai.

Licha ya kutokuwa na ustadi wa kuchonga vinyago lakini Mbithe anadhihirisha kuwa kiungo muhimu katika kazi hii akitia nakshi vinyago kabla ya kuuzwa.

Na mara Akilimali ilipomsogelea karibu kutaka kujua mengi kuhusu kazi yake, Mbithe anatabasamu mwanzo kisha kunikaribisha kwa moyo mkunjufu.

“ Hapa ni kazi tu, hatubagui wala kuchagua bora iwe halali na inayotuwezesha kuweka chakula mezani,” asema Mbithe Reuben mara alipoanza mahojiano na Akilimali.

Mbithe ni kati ya wanawake wachache wenye uzoefu na ustadi mkubwa katika wa kutia nakshi vinyago katika karakana hii iliyo mkabala na kituo cha Polisi cha Changamwe.

Ni kazi ambayo ameifanya kwa takribani miaka 19 bila kuchoka mara baada ya kukamilisha masomo yake ya msingi ya Misuuni, Mtito Andei.

Kulingana na Mbithe, hakuweza kuendeleza masomo yake ya upili kutokana na hali ya uchochole iliyokuwa ikiing’ata familia yake kipindi hicho.

Aliamua kuelekea Mombasa kusaka njia mbadala ya kuikwamua familia yake ijapo alifahamu fika elimu yake haingemruhusu kupata kazi yenye mapato mazuri.

BIASHARA NDOGONDOGO

Mara alipowasili Mombasa katika mtaa wa Chaani, hakuwa na muda wa kuchagua kazi na mara moja akajitosa katika kazi ya kuwafulia watu nguo kwa malipo.

Kutokana na kazi hiyo, Mbithe alipata mtaji wa kuanzisha biashara ya kuuza nguo za mitumba akizunguka mitaani.

Hata hivyo, kazi hiyo ilikuwa na changamoto zake hivyo Mbithe akashauriwa na rafikiye kujaribu ya kutia nakshi vinyago .

“ Mwanzoni nilisita kukubali kutokana na kazi hiyo kumilikiwa na wanaume na ikizidi sikuwa na ufahamu katika kazi hiyo lakini nikajipiga moyo konde kujaribu,’ asimulia Mbithe.

Lakini baada ya kufunzwa jinsi ya kufanya kazi hiyo, aliweza kuhitimu vyema baada ya kipindi cha miezi miwili kutokana na kujituma kwake kazini.

“ Wachongaji vinyago walianza kunimini kutokana na kasi yangu iliyokuwa ya kipekee hivyo wakaniletea kazi kwa wingi,” asema.

Mbithe anaifichulia Akilimali kwamba siri ya mafanikio yake katika kazi hii ni nidhamu na kujituma kila wakati.

Kulingana na Mbithe kwa siku ana uwezo wa kutia nakshi vinyago 70 ama hata 100 na kutia kibindoni kitita cha kati ya Sh1,000 hadi 1,500.

Ustadi wa Mbithe katika kutia nakshi vinyago kila sampuli umemzolea sifa kedekede ambapo imekuwa nadra kwake kukosa kupata oda ya kazi kutoka kwa wachongaji vinyago katika karakana zilizoko karibu eneo la Changamwe.

 

Vinyago ambavyo vimetiwa nakshi tayari kuuzwa. Ni kazi ya Mbithe Reuben mama mwenye umri wa miaka 38 ambaye ni stadi wa kutia nakshi vinyago kila sampuli katika karakana ya uchongaji vinyago iliyoko Changamwe, Mombasa. PICHA ZOTE/CHARLES ONGADI

MANUFAA

Kutokana na kipato anachovuna kutokana na kazi yake, amefaulu katika kubadilisha maisha ya wazazi wake mashambani huku ikimwezesha kuwapatia watoto wake kupata elimu bora na wala siyo bora elimu.

“ Mapato kutoka kazi yangu imeniweza kunikimu kimaisha na namshukuru sana rafiki yangu aliyenifunza kazi hii ,” asema Mbithe.

Anaongeza kwamba kazi kibao zipo nchini ila endapo mtu atakuwa mbunifu na kujituma kila mara ili kufikia malengo.

CORONA YAZUA BALAA

Kulingana na Mbithe, mlipuko wa virusi vya Corona umeyumbisha kwa kiasi kikubwa kazi yake kutokana na kwamba wateja wao wakuu ambao ni watalii kutoka nchi za ughaibuni hawaji nchini kama ilivyokuwa zamani.

Anasema ni wateja wachache sana wanaozuri karakana yao kununua vinyago kutokana na janga la maambukizi ya virusi vya Corona.

“ Zamani wateja wengi walionekana eneo hili wakinunua vinyago kupeleka nchi za ughaibuni lakini wateja waliobaki kwa sasa ni wananchi wenyewe,” asema.

Hata hivyo, anaamini kidogo anachopata kwa sasa kinamwezesha kusukuma gurudumu la maisha bila kumtegemea yeyote .

Anawashauri akina mama kutochagua kazi bali wafanye tu ile halali inayopatikana ili kuweza kushirikiana na mabwana katika kulea familia.

CHANGAMOTO

Kulingana na Mbithe, swala la ukosefu wa kazi limepelekea baadhi ya wanaume kujitosa katika kazi hii hivyo kuleta upinzani mkali na kutatiza kipato chake cha kila siku.

Lakini Mbithe anaamini bidii na usanifu wake mkubwa katika kufanya kazi yake imezidi kuwatia imani wachongaji vinyago ambaohaweshi kumpatia kazi kila siku.

Hata hivyo, anakiri kwamba kutokana na ugumu wa maisha kwa sasa kuna kipindi anarudi nyumbani mikono mitupu ama kiasi kidogo cha hela.

Anaamini hivi karibuni hali itarudi sawa na biashara yake kunoga tena kama ilivyokuwa zamani.

You can share this post!

Madiwani wa Nyeri watiwa presha wapitishe BBI

MAUYA OMAUYA: Nyachae alikuwa na bidii, ila alikuwa...