HabariSiasa

ADA YA UJENZI: Atwoli atasaliti wafanyakazi?

May 1st, 2019 2 min read

Na LEONARD ONYANGO

WAKENYA wanasubiri kwa hamu na ghamu kuona ikiwa Rais Uhuru Kenyatta atabadili msimamo wake kuhusiana na ada ya Mpango wa Kitaifa wa Ujenzi wa Nyumba katika hotuba yake ya Leba Dei.

Ushuru huo umepingwa vikali na mashirika mbalimbali yakiwemo Chama cha Wanunuzi Bidhaa Kenya (Cofek), Chama cha Walimu (Knut), Muungano wa Waajiri (FKE), kati ya mashirika mengineyo.

Katibu Mkuu wa Cotu Francis Atwoli, hata hivyo, amebadili msimamo wake na kukubali wafanyakazi watozwe ada hiyo kwa sharti moja: Rais Kenyatta atangaze nyongezeko ya mshahara wa wafanyakazi wa chini kwa asilimia 15.

Lakini kile Wakenya wengi wanatilia shaka ni utekelezaji wa agizo la rais kuhusu nyongeza ya mishahara. Mbeleni, waajiri wameripotiwa kukaidi nyongeza hiyo kwa kisingizio kuwa nyongeza kama hiyo italemaza mashirika yao.

Hivyo basi, kuna wale wanaoamini kuwa, kwa misingi hiyo, Bw Atwoli alisaliti wale anaowawakilisha kwa kutoa masharti hafifu kama hayo.

Serikali inapanga kuwatoza wafanyakazi walioajiriwa asilimia 1.5 ya mishahara yao kama ada ya mpango huo.

“Mpango wa Kitaifa wa Ujenzi Nyumba ni mzuru kwa kuwa wengi watanufaika. Tumeitaka serikali kuongezea wafanyakazi wa malipo ya chini mshahara kwa asilimia 15 ili tuunge mkono ada hiyo mpya,” akasema Bw Atwoli wiki iliyopita.

Mnamo Septemba 2018, muungano wa Cotu ulikataa ada hiyo ukisema kuwa wafanyakazi hawakushauriwa kinyume na matakwa ya katiba.

Serikali ilifaa kuwatoza wafanyakazi ada hiyo kuanzia mwezi huu kabla ya kusimamishwa na mahakama.

Jaji Maureen Onyango alitoa agizo hilo, akisema kusimamishwa kutozwa kwa ada hiyo kutatoa nafasi ya kuunganishwa kwa kesi zilizowasilishwa kortini na Cofek na Cotu.

Ikiongozwa na Katibu Mkuu wake Stephen Mutoro, Cofek inashikilia utekelezaji wa mpango huo utawaongezea Wakenya mzigo wa ushuru mkubwa wanaotozwa na serikali.

“Si haki kuwashinikiza wananchi kuchangia mpango wa nyumba ambazo huenda zisiwafaidi baadaye,” ikasema kwenye malalamishi yake.

Kupitia wakili Henry Kurauka, Cofek pia ilisema si Wakenya wote walioweka umiliki wa nyumba kuwa suala muhimu kwao, hivyo hawapaswi kulazimishwa kuuchangia.

Kiongozi wa Chama cha Amani National Congress (ANC) Musalia Mudavadi pia alipinga mpango huo akisema, Wakenya wengi wanakabiliwa na hali ngumu ya maisha.

“Kutokana na hali ngumu ya maisha na kiangazi kinachoendelea, haifai hata kidogo kumwongezea mwananchi mzigo mwingine wa ushuru,” akasema Bw Mudavadi kwenye kikao na waandishi, jijini Nairobi wiki iliyopita.

Mahakama ya Masuala ya Leba ilikuwa imesimamisha utekelezaji wake hadi Mei 20, ambapo kesi ingeanza kusikizwa kikamilifu.

Chama cha Knut kupitia kwa Katibu Mkuu wake Wilson Sossion, kimeshikilia kuwa walimu hawatakubali kutozwa ushuru huo hadi serikali itakapowaongeza zaidi ya asilimia tisa ya mishahara yao.

Serikali inalenga kujenga nyumba 500,000 za bei rahisi kufikia 2022.

Wakenya walionekana kutilia shaka mpango huo baada ya Katibu katika Wizara ya Ujenzi anayehusika na miundomsingi, Bw Charles Hinga, kusema watakaobahatika kuzipata ni wale watakaochaguliwa kwa mfumo wa bahati nasibu.