Habari Mseto

Ada za kutuma pesa kwa simu zarejea Januari

December 17th, 2020 2 min read

Na PAUL WAFULA

UTAKUWA mwezi mgumu wa Januari kwa Wakenya baada ya Benki Kuu ya Kenya (CBK) Alhamisi kurejesha ada za kutuma Sh1,000 kwenda chini kwa njia ya simu, ambazo zilikuwa zimefutiliwa mbali.

Benki ilitangaza kufutilia mbali ada hizo mwezi Machi ili kuwasaidia Wakenya kuhimili athari za kiuchumi za janga la virusi vya corona.

Hatua hiyo inajiri baada ya Wizara ya Fedha kutangaza kurejeshwa kwa viwango vya awali vya kodi ambavyo Wakenya walikuwa wakitozwa kabla ya janga hilo.

Awali, ada hizo zilikuwa zimeondolewa hadi Juni 30 mwaka huu, lakini muda huo ukaongezwa hadi Desemba 31, baada ya serikali kufanya tathmini.

Kutokana na hatua hiyo, kampuni ya Safaricom ililalama kwamba ingepoteza mapato ya hadi Sh19 bilioni kufikia mwishoni mwa mwaka.

Mwezi uliopita, kampuni hiyo ilitangaza hasara ya Sh2 bilioni, baada ya faida yake kupungua kutoka Sh35 bilioni mwaka 2019 hadi Sh33 bilioni.

Kampuni hiyo ilisema mapato kutokana na utumaji pesa kupitia kwa njia ya M-Pesa yalipungua kwa kiwango cha Sh6.1 bilioni.

“Hali yetu ya biashara imeathirika, ijapokuwa tunaamini mambo yataimarika licha ya athari za janga la corona. Janga hili limemwathiri kila mmoja,” akasema Afisa Mkuu Mtendaji, Bw Peter Ndegwa wakati akitoa matokeo hayo.

Benki na kampuni nyingine za kutoa huduma za kutuma pesa kwa njia ya simu pia zimekuwa zikipitia hali ngumu.

Kwenye tangazo lake, CBK ilisema ilichukua hatua hiyo baada ya kushauriana na wadau wote husika.

Hata hivyo, ada hizo hazitakuwa zikitozwa wale watakaokuwa wakituma kiwango Sh100 kwenda chini katika mtandao wowote.

Mapema Desemba, Waziri wa Fedha, Bw Ukur Yatani alisema kuwa kuondolewa kwa baadhi ya masharti ya kudhibiti corona ambayo yalikuwa yamewekwa na serikali ndiko kumewalazimu kurejesha ada za kawaida za ushuru kutoka Januari 1, 2021.

Ushuru ambao kampuni hutozwa kutokana na faida zao utarejea kuwa asilimia 30 kutoka asilimia 25, nao ushuru ambao wafanyakazi hutozwa kwenye mishahara yao utarejea kuwa asilimia 30 kutoka asilimia 25 kwa sasa.

Ushuru ambao hutozwa bidhaa nao utarejea asilimia 16 kutoka asilimia 14 kwa sasa.

Benki hiyo ilisema itaruhusu wanaotuma pesa kwa njia ya simu kuendelea kutuma chini ya kanuni za sasa hadi Desemba 31, lakini masharti mapya yatatolewa kuanzia Januari 1.

Kwenye taarifa yake, benki hiyo ilisema kutokana na kuondolewa kwa ada hizo, kiwango cha pesa zilizotumwa kwa njia ya simu kiliongezeka sana, hilo likionyesha hatua hiyo ilikuwa afueni kwa Wakenya wengi.

Kwa mfano, kati ya mwezi Februari na Oktoba, kulikuwa na ongezeko la Wakenya 2.8 milioni walioanza kutumia njia ya simu kutuma pesa zao.

“Wakenya pia walitumia njia hiyo pakubwa kwa huduma za kibiashara. Tumetathmini kuhusu hatua tulizopiga na mafanikio tuliyopata kupitia kanuni hizo. Lengo letu ni kuhakikisha kuwa tumerejea katika hali ya kawaida kwa taratibu zifaazo,” ikasema benki hiyo.