Siasa

Adai wanasiasa wa nje huvuruga Pwani

December 13th, 2020 2 min read

Na FADHILI FREDRICK

GAVANA wa Kilifi Amason Kingi amelalamika kuwa wanasiasa kutoka nje ndio wamekuwa wakivuruga nia ya wakazi wa Pwani kuungana kisiasa kwenye chaguzi zilizopita.

Bw Kingi alidai kuwa wanalenga kufufua mjadala wa umoja wa Wapwani baada ya uchaguzi mdogo wa eneobunge la Msambweni ambao utafanyika hapo kesho.

Mbunge huyo wa zamani wa Magarini aliwalaumu wanasiasa kutoka nje ya ukanda huo kwa kuvuruga mipango yao ya kila mara ya kuungana ili waendelee kunufaika kisiasa na mgawanyiko huo.

“Tutafufua mjadala wa Wapwani kuungana baada ya uchaguzi mdogo kwa kuwa tunalenga kuunda serikali ijayo. Tupo tayari kuhakikisha kuwa mara hii tunaungana kutoka Vanga hadi eneo la mpakani katika Kaunti ya Lamu,” akasema Bw Kingi akihutubia mkutano wa kisiasa katika kijiji cha Nganja.

Alikuwa akimpigia debe mwaniaji wa ODM kwenye uchaguzi huo Omar Iddi Boga ambaye atapambana na mwaniaji wa kujitegemea Feisal Bader anayeungwa mkono na mrengo wa Naibu Rais Dkt William Ruto.

Gavana huyo ambaye alikuwa ameandamana na wabunge William Kamoti (Rabai) na Mishi Mboko (Likoni) alitoa wito kwa wakazi wajitokeze kwa wingi kumpigia kura Bw Boga wakimtaja kama anayetosha kuvaa viatu vya marehemu Suleiman Dori aliyefariki Machi mwaka huu.

Aidha Bw Kingi alisisitiza kuwa yupo makini kuhakikisha tatizo kubwa kuhusu umiliki wa ardhi katika eneobunge la Msambweni linatatuliwa akiahidi kushirikiana na Bw Boga kutimiza hilo.

“Shida kubwa hapa ni utata kuhusu umiliki wa ardhi. Kampuni nyingi zimetwaa ardhi na kuwatishia wenyeji na hili ni jambo ambalo linahitaji mbunge jasiri kama Bw Boga wala si yule mwingine,” akaongeza Bw Kingi.

Alisisitiza kuwa Bw Boga ni mwaniaji ambaye anaungwa mkono na Rais Uhuru Kenyatta na Kinara wa ODM Raila Odinga, akisema ndiye chaguo bora ambaye atatua shida za wanaeneobunge hilo.

Huku Bw Kingi akimvumisha Bw Boga kwenye wadi ya Ramisi na Kinondo, wandani wa Dkt Ruto wakiongozwa na Gavana Salim Mvurya walikuwa ukunda wakimpigia kampeni kali Bw Bader.

Bw Mvurya alisema kuwa kampeni ambazo zimekuwa zikiendeshwa na ODM zilijaa vitisho akishangaa kwa nini viongozi wa chama hicho walikuwa wakisisitiza lazima washinde uchaguzi huo.

“Inaonekana ODM wanapanga wizi wa kura. Hiyo ndiyo maana wana uhakika wa kupata ushindi,” akasema Gavana huyo.

Vile vile Bw Mvurya alitoa wito kwa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) iwe makini ili kuzuia wizi wa kura akisema hataruhusu wakazi wa Msambweni wanyimwe haki zao za kikatiba.

Naibu Gavana Fatuma Achani naye aliwakashifu viongozi wa ODM kwa kutowaheshimu viongozi waliochaguliwa katika kaunti ya Kwale wakati wa kampeni hiyo.

Viongozi hao wawili pia waliapa kuwa watazilinda kura za Bw Bader wakieleza matumaini yao kwamba atashinda na kuwa mbunge.