Kimataifa

Adaka mkwanja wa Sh150 bilioni kwenye jackpot ya kamari

October 25th, 2018 1 min read

MASHIRIKA na PETER MBURU

MAREKANI

MTU mmoja ameshinda dola 1.5 bilioni za Marekani kwenye mchezo wa Kamari, baada ya kununua tiketi yenye nambari sita zilizooana na zilizotangazwa kwenye mchezo wa Jumanne usiku.

Mtu huyo alijishindia hela hizo baada ya kuambatanisha nambari 5,28,62,65,70 na mpira mkubwa nambari 5, ushindi ambao ulikuwa na nafasi moja kati ya nafasi 302.5milioni kwa mtu kushinda.

Mchezo huo wa Kamari huchezwa katika majimbo 44 ya Marekani, yakiwemo Washington, DC na visiwa vya Virgin.

Maafisa wa kampuni hiyo ya Kamari walitangaza kuwa jakipoti hiyo ilishindwa baada ya tiketi ya nambari hizo kununuliwa, jambo lililowashangaza wengi.

Washindi wa Kamari hiyo hupewa kati ya siku 180 hadi mwaka kudai tuzo yao kulingana na jimbo wanalotoka, na hivyo mshindi huyo anatarajiwa kuchukua siku kadha kabla ya kujitokeza.

Katika majimbo ya Delaware, Georgia, Kansas, Maryland, North Dakota, Ohio, South Carolina na Texas, washindi wanawezakusalia bila kutambulishwa, lakini majimbo mengine washindi hutangazwa.

Mshindi huyo sasa ameshinda baada ya miezi mitatu ya mchezo huo kukosa mshindi, jambo lililokuza pesa hizo kwa kiwango kikubwa.

Mara ya mwisho kwa jakipoti hiyo kushindwa ilikuwa  Julai 24 wakati wafanyakazi 11 wa kampuni moja California walishinda tuzo ya dola 543milioni.

Jakipoti hiyo inasemekana kuwa kubwa zaidi katika historia ya Marekani.

Wacheza Kamari walikuwa wakipiga foleni ndefu katika maeneo ya huduma za kampuni hiyo ili kupata nafasi ya kushinda tuzo hiyo bila kufanikiwa.

“Wakati ambao tumekuwa tukisubiri hatimaye umewadia, na tumefurahi sana,” akasema Gordon Medenica, Mkurugenzi Mkuu wa kampuni ya Mega Millions Group.

“Hiki ni kisa cha kihistoria. Tumefurahi sana kwa mshindi na kampuni ya Kamari ya South Carolina inasubiri kukutana na mshindi.”

Lakini huenda umma usimjue mshindi huyo kwa kuwa jimbo la South Carolina huwa si lazima kwa mshindi kutambulishwa.

Mshindi huyo sasa ataamua ikiwa atapokea dola 913milioni baada ya kutozwa ushuru, ama alipwe polepole kwa miaka 29.