Michezo

ADAKA yawarai Wakenya kuzidisha vita dhidi ya pufya

January 15th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

SHIRIKA la Kukabiliana na matumizi ya dawa za kusisimua misuli michezoni nchini (ADAK) limeomba Wakenya kujitokeza hata zaidi kuunga mkono vita dhidi ya uovu huo unaoweka Kenya pabaya.

Kupitia mtandao wake wa kijamii Jumatatu, ADAK imehakikishia usalama mtu yeyote atakayeiwasilishia habari muhimu zitakazopiga jeki vita hivi.

“Tukiwa katika mwaka mpya, tunaendelea na kukuomba uchangie katika vita dhidi ya matumizi ya dawa za kusisimua misuli. Tupe habari zozote zitakazotusaidia kuendeleza juhudi zetu za kuhakkisha mashindano ni safi nchini Kenya: Kuwa mwanajeshi katika vita dhidi ya matumizi ya pufya.

Ripoti kisa chochote cha matumizi ya dawa za kusisimua kupitia baruapepe[email protected]. Hatutakufichua,” shirika hilo limetangaza.

Mwito wa ADAK unawasili wiki chache baada ya Rais wa Shirikisho la Riadha la Kenya (AK) Jackson Tuwei kuomba wanariadha wajitenge na njia ya hii ya mkato ya kupata ufanisi ili kuokoa sifa ya Kenya.

Alijuta kwamba Kenya inaendelea kabisa kukaribia kupigwa marufuku na Shirikisho la Riadha Duniani (IAAF) kwa sababu watumiaji wa dawa hizo haramu mashindanoni wameongezeka.

“Kwa miaka minne mfululizo, tumekuwa katika orodha ya IAAF ya mataifa ambayo yamekuwa yakichunguzwa sana. IAAF sasa imetuweka katika orodha ya mataifa yanayokodolea macho kupigwa marufuku (Kategoria A),” alisema Tuwei huku akifichua kwamba udanganyifu wa umri pia ni tatizo kubwa.

Kuhusu matumizi ya dawa za kusisimua misuli ni kwamba tangu mwaka 2012. Kenya imeshuhudia zaidi ya visa 50 vya uhalifu wa kutumia dawa zilizopigwa marufuku kujitafutia ufanisi mashindanoni.

Baadhi ya majina makubwa yaliyoingia katika orodha ya watumiaji wa dawa hizo mwaka 2018 ni bingwa wa dunia na Olimpiki wa mbio za mita 1,500 Asbel Kiprop, mtimkaji wa mbio fupi za mita 400 Boniface Mweresa na malkia wa mbio za mita 10, 000 za Jumuiya ya Madola mwaka 2006, Lucy Wangui Kabuu, ambaye tangu mwaka 2011 amekuwa akijaribu bahati yake katika mbio za kilomita 21 na kilomita 42.

Mataifa mengine yanayopatikana katika Kategoria A ni Ethiopia, Belarus na Ukraine. Mwezi Desemba mwaka 2018, India pia ilitiwa katika kundi hili kutokana na kwamba zaidi ya wanaspoti wake 100 wamegunduliwa wakitumia uovu huu kufaulu mashindanoni tangu mwaka 2012.

Urusi imekuwa ikitumikia marufuku kutoka kwa IAAF tangu mwaka 2015 baada ya visa vingi kugunduliwa pamoja na serikali ya nchi hiyo kupatikana ilifadhili wanamichezo kutoka fani mbalimbali kutumia njia hii ya mkato.