Michezo

Adebayor apuuza wanaomshinikiza kutoa mabilioni kupigana na corona

April 24th, 2020 1 min read


Na GEOFFREY ANENE

NAHODHA wa zamani wa timu ya taifa ya Togo, Emmanuel Adebayor, amepuuzilia mbali wanaotaka amege sehemu ya mali yake ya Sh4.8 bilioni kusaidia katika vita dhidi ya janga la corona nchini mwake.

Adebayor, ambaye alipata umaarufu akisakatia soka Arsenal nchini Uingereza kabla ya kuvalia jezi za Manchester City, Real Madrid, Tottenham Hotspur, Crystal Palace, Istanbul Basaksehir na Kayserispor barani Ulaya, ni mchezaji wa Olimpia Asuncion nchini Paraguay.

Mshambuliaji huyu, ambaye pia ana uraia wa Nigeria, alijiunga na klabu hiyo ya Paraguay wiki mbili kabla asherehekee kufikisha umri wa miaka 36 mwezi Februari kwa kandarasi itakayokatika Desemba 31, 2020.

Amenukuliwa na vyombo vya habari akisema hawezi kutoa hata ndururu kusaidia katika vita hivyo kwa sababu si yeye alileta virusi hivyo nchini Togo.

“Kwa wale wanaosema kuwa mimi sitoi mchango, acha niwaambie kuwa mimi kweli huwa sitoi. “Nitafanya kile nataka kufanya, kula chakula ninachotaka, na kwangu hii ndio muhimu sana. Kisha, kutakuwepo na wale wakosoaji wangu, ambao wanasema sijaanzisha shirika la kusaidia wenye shida nchini Togo.

“Hata hivyo, inaonekana kama kwamba mimi ndio nilileta virusi vya corona Togo, hicho si kitu kizuri… Poleni kwa wale wanaonilinganisha na Samuel Eto’o (Cameroon) na Didier Drogba (Ivory Coast) wakisema kuwa sina wakfu ama mbona sisaidii kama kwamba mimi nilileta virusi vya corona nchini Togo.” Togo imeshuhudia visa 88 vya maambukizi ya virusi hivyo, huku watu sita wakipoteza maisha yao kutokana na virusi hivyo.