Michezo

Ademola Lookman ajiunga na Fulham kwa mkopo kutoka RB Leipzig

October 1st, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

FULHAM wamemsajili fowadi wa zamani wa Everton, Ademola Lookman kwa mkopo wa mwaka mmoja kutoka RB Leipzig ya Ujerumani.

Lookman, 22, anarejea sasa katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kuingia katika sajili ya Leipzig kutoka Everton kwa kima cha Sh3.1 bilioni mwanzoni mwa msimu wa 2019-20.

Kwa mujibu wa sogora huyo raia wa Uingereza, maamuzi ya kutua Fulham ni zao la kushawishiwa pakubwa na kocha wa kikosi hicho, Scott Parker.

“Baada ya mazungumzo na Parker, nilihiari kurejea EPL. Kubwa zaidi ni uhusiano bora ambao umekuwepo kati yangu naye,” akasema Lookman.

“Ni mwanasoka mchanga aliye na kiu ya kukua kitaaluma. Nami nimeridhishwa na kiwango cha ubora wake. Ni tija kubwa kwamba alikubali kujiunga nasi,” akasema Parker.

Katika msimu wake wa kwanza kambini mwa Leipzig, Lookman alipachika wavuni mabao matano kwenye mechi 11 za Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) tangu apokezwe mkataba wa kudumu kambini mwa Leipzig mnamo Julai 2019.

Fulham ambao wamerejea katika EPL msimu huu, wamepoteza jumla ya michuano mitatu ya ufunguzi wa msimu huu na ujio wa Lookman ni mojawapo ya mikakati ya kusukwa upya kwa kikosi hicho chini ya Naibu Mwenyekiti, Tony Khan.

Khan aliwaomba radhi mashabiki wa Fulham kwa kichapo cha 3-0 walichopokezwa na Aston Villa mnamo Jumatatu ugani Craven Cottage.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO