Adhabu ya kiboko shuleni yapingwa

Adhabu ya kiboko shuleni yapingwa

Na CHARLES WASONGA

PENDEKEZO la Wizara ya Elimu kwamba adhabu ya viboko irejeshwe shuleni kama njia ya kudhibiti utundu miongoni mwa wanafunzi, liliendelea kupingwa jana na wadau katika sekta ya elimu.

Kanisa la Kianglikana nchini na vyama vya kutetea masilahi ya walimu nchini vilisema suluhu kwa tatizo hilo ni wazazi kuzingatia kwa makini wajibu wao kama walezi na washauri wa watoto wao.

Kasisi wa Kanisa la All Saints Cathedral, Nairobi, Sammy Wainaina alisema visa vya utovu wa nidhamu na uteketezaji wa mali ya shule vinavyoshuhudiwa katika shule kadha za upili ni kielelezo cha utovu wa maadili na malezi bora katika familia.

“Isitoshe, watoto wetu wanasababisha fujo shule kwa kuiga yale yanayoendelea katika familia, jamii na taifa kwa ujumla kwamba tukitofautiana, tunapigana.

“Kwa hivyo, suluhu kwa tatizo hilo sio kurejesha adhabu ya viboko shuleni bali ni wazazi na wanajamii kuwa kielelezo bora kwa watoto wetu kwa kupalilia maadili na mbinu za kutatua mizozo kwa amani,” akasema alipoongoza ibada ya Jumapili katika kanisa hilo.

“Kumchapa mwanafunzi hakusuluhisha tatizo hili. Wazazi wanafaa kutekeleza wajibu wao wa kuwa walezi na washauri wa kwanza wa watoto wao. Wajibu huu usiachiwe walimu,” Kasisi Wainaina akaongeza akisema “kurejeshwa kwa adhabu ya viboko kutapelekea hali hii kuwa mbaya zaidi.”

Naye Katibu Mkuu wa Chama cha Kitaifa cha Walimu (Knut) Wilson Sossion amepinga pendekezo la kuwachapa wanafunzi watundu kwa viboko akisema, badala yake shule za mabweni zinapasa kupigwa marufuku ili kutoa nafasi kwa wazazi kuwa na wakati mwingi wa kuwatunza watoto wao.

Alisema kurejelewa kwa adhabu hiyo kutagonganisha wanafunzi, wazazi na walimu, hali ambayo itaathiri masomo.

“Vile vile, hatua hiyo huenda ikapelekea wanafunzi kuwageukia walimu wao, kuwadhuru na hata kuwaua. Tukio kama hili tayari limetokea katika Shule ya Pili ya Kitaifa ya Kisii ambapo wanafunzi waliwashambuliwa walimu wao kwa visu.

Hatutaki shule zetu kugeuzwa uwanja wa vita kati ya walimu na wanafunzi,” Bw Sossion akasema Jumamosi alipohudhuria uchaguzi wa Knut, tawi la Nakuru.

You can share this post!

Ruto alia ‘mahasla’ wanamfyonza

Raila atetea Uhuru kuhusu mapungufu ya Jubilee