Adhabu ya Onana aliyepigwa marufuku kwa miezi 12 yapunguzwa kwa miezi mitatu zaidi

Adhabu ya Onana aliyepigwa marufuku kwa miezi 12 yapunguzwa kwa miezi mitatu zaidi

Na MASHIRIKA

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

MARUFUKU ambayo kipa Andre Onana alikuwa amepigwa kwa hatia ya kutumia dawa za kusisimua misuli yamepunguzwa na Jopo la Kimataifa la Malalamishi ya Spoti (CAS) kutoka miezi 12 hadi miezi tisa.

Nyota huyo mwenye umri wa miaka 25 alikuwa ameadhibiwa na Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa) mnamo Februari baada ya vipimo vya afya alivyofanyiwa mnamo Oktoba 30, 2020 kubainisha kwamba sampuli za mkojo wake zilipatikana na chembechembe za dawa haramu aina ya furosemide.

Hata hivyo, Ajax walisisitiza kwamba Onana alimeza kimakosa dawa zilizokuwa za mkewe alipougua mwanzoni mwa mwezi huo wa Oktoba 2020.Onana aliwasilisha rufaa kwenye jopo la CAS akitaka maamuzi hayo ya Uefa kubatilishwa.

Kupitia taarifa aliyoituma kwa vyombo vya habari, Onana alisema aligundua kwamba alikuwa amemeza dawa zilizokuwa za mkewe kwa kudhani kwamba ni aspirin alizokuwa ameagizwa na daktari wake kutumia.

Kosa alilolifanya lilichangiwa na kushabihiana kwa boksi zilizokuwa na dawa hizo mbili – yake na ya mkewe.Hadi alipopigwa marufuku, Onana ambaye kwa sasa anamezewa na Arsenal, hakuwa amefungwa bao lolote kwenye mechi 20 za Ligi Kuu ya Uholanzi (Eredivisie) msimu wa 2020-21.

Maamuzi ya CAS yanamaanisha kwamba marufuku ya Onana sasa yatakamilika mnamo Novemba 4, 2021 na hivyo atakosa kuwa sehemu ya kampeni za Ajax mwanzoni wa msimu ujao. Hata hivyo atarejea kudakia Cameroon ambao watakuwa wenyeji wa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) mnamo Januari 2022.

Atakosa pia mechi za kufuzu kwa fainali zijazo za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar ambazo zitakutanisha Cameroon na Malawi na Ivory Coast mnamo Septemba kisha Msumbuji mnamo Oktoba 2021.Huku akizuiwa kucheza mechi zozote za kitaifa na kimataifa hadi Novemba 4, Onana ana kibali cha kurejelea mazoezi mnamo Septemba 4, miezi miwili kabla ya marufuku dhidi yake kukamilika.

 

  • Tags

You can share this post!

Mkulima anavyochuma kwa mimea na ufugaji samaki

Wijnaldum aondoka Liverpool na kuingia PSG kwa mkataba wa...