Dondoo

Adhani kapata mke kumbe kicheche

July 7th, 2019 1 min read

 Na John Musyoki

KIAMBERE MJINI

KALAMENI mmoja mjini hapa alijuta baada ya demu aliyemkaribisha kwake kumuibia pesa na simu.

Duru za mtaani zinasema kuwa jamaa alipenda kuwatongoza akina dada mtaani kila mara akilipwa mshahara. Siku chache kabla ya kioja, alifika kwake mwanadada mrembo na kujulisha majirani kwamba alikusudia kumuoa.

“Mwaonaje huyu mrembo? Kwa sasa sina haja ya kuwafuata wanawake wengine. Huyu ni tosha na tena mpole sana. Nitamuoa hivi karibuni kwa hivyo kila mmoja awe tayari kuhudhuria harusi yetu,” jamaa alisikika akijigamba.

Yasemekana baadhi ya marafiki wa jamaa walimpongeza kwa kufanya uamuzi wa busara japo wengi wao walimkosoa kwa kutaka kumuoa demu huyo ilhali hakuwa amemfahamu kwa muda mrefu.

“Utafanya vizuri ukioa kwa sababu tabia unayofanya ya kubadilisha wanawake itakutia matatani lakini mchunguze sana kabla hajakuwa mke wako. Hapa ni mjini na wanawake wengi sio wa kuaminika,” mama mmoja alimwambia jamaa.

Jamaa kwa kiherehere chake, alipuuza ushauri wa busara wa mama huyo.

“Sasa umeamua kunitoa nyama mdomoni. Mwanadada huyu ni mrembo sana na tena namwamini, hawezi kuwa kigeugeu kama wanawake wengine,” jamaa alijibu.

Usiku wa manane siku hiyo, jamaa alisikika akilalamika baada ya kumkosa mwanadada huyo chumbani.

“Huyu ameenda wapi? Kwani yeye ni jini ama ninaota. Pesa zangu na simu haziko,” jamaa alisikika akilalamika.

Inasemekana alitoka chumbani na kuanza kuangua kilio huku akijuta baada ya kupuuza ushauri wa mwenzake.

“Naota ama kulikoni? Ako wapi mrembo niliyekuwa naye chumbani?” jamaa alilia na kuwaamsha majirani.

“Ndugu yangu hauoti. Huu ndio ukweli wa mambo. Nilikuambia ukadhani ni ndoto. Sasa unajuta,” mama aliyemshauri awali alimweleza.