Michezo

Aduda apendekeza Bandari FC wapewe fursa kuwakilisha Kenya kwenye CAF Confederations Cup msimu wa 2020-21

September 8th, 2020 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

ALIYEKUWA Afisa Mkuu Mtendaji wa Gor Mahia, Lordvick Aduda, ametaka Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kuwapa Bandari FC fursa ya kuwakilisha taifa kwenye Kombe la Mashirikisho barani Afrika (CAF Confederations Cup) katika msimu wa 2020-21.

Mnamo Septemba 1, 2020, Shirikisho la Soka la Afrika (CAF) lilitaka mataifa yote wanachama wa CAF kuwasilisha majina ya wanasoka na klabu zitakazopeperusha bendera zao kwenye kivumbi hicho kufikia Oktoba 20.

FKF tayari iliwasilishia CAF jina la Gor Mahia ambao watawakilisha Kenya kwenye Klabu Bingwa barani Afrika (Champions League) baada ya kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya KPL mwishoni mwa msimu wa 2019-20.

Hata hivyo, FKF haikutoa mwakilishi wa Confederations Cup baada ya janga la corona kuchangia kusitishwa ghafla kwa kipute FKF Shield Cup kilichokuwa kimefikia hatua ya 16-bora. Mshindi wa kivumbi hicho ndiye huwakilisha Kenya katika mapambano ya kimataifa ya CAF.

Aidha, Katiba ya FKF haina utaratibu wa kuiwezesha kutoa mwakilishi wa Kenya kwenye Confederations Cup iwapo kampeni za Shield Cup hazitakamilika na mshindi kupatikana.

“Bandari ndio mabingwa watetezi wa Shield Cup. Waliwakilisha Kenya vyema kwenye michuano ya CAF na wakawa pua na mdomo kutinga hatua ya makundi baada ya kuwaangusha miamba,” akatanguliza Aduda.

“Hatuwezi kuipoteza nafasi hii. Mbali na kujivunia uwezo mkubwa wa kifedha, Bandari pia watapata uzoefu zaidi katika soka ya kimataifa na hivyo kuinua kiwango cha maendeleo ya wanasoka wao kitaaluma,” akaongeza.

Kwingineko, fowadi matata wa KCB, Enock Agwanda, amefutilia mbali tetesi zinazomhusisha na uwezekano wa kutua Zambia kuvalia jezi za Red Arrows FC.

Awali, Agwanda alikuwa akihusishwa pakubwa na Napsa Stars ambao sasa wamemsajili aliyekuwa fowadi mahiri wa Tusker, Timothy Otieno kwa mkataba wa miaka miwili.

“Ningali na miezi sita zaidi kwenye mkataba wangu wa sasa na KCB. Sijapokea ofa yoyote ya kujiunga na klabu inayoshiriki Ligi Kuu ya Zambia,” akasema nyota huyo wa zamani wa SoNy Sugar katika kauli iliyoungwa na kocha msaidizi wa KCB, Godfrey Oduor.

Kwa mujibu wa Agwanda, kubwa zaidi katika maazimio yake ni kurejea katika timu ya taifa ya Harambee Stars itakayotegemewa na kocha Francis Kimanzi katika kibarua kijacho dhidi ya Comoros kwenye jitihada za kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) za 2021.

Stars wametiwa pia kwenye zizi moja na Mali, Uganda na Rwanda kwenye mechi zitakazopigwa kati ya Mei 2021 na Novemba 2021 katika juhudi za kufuzu kwa fainali za Kombe la Dunia za 2022 nchini Qatar.