Michezo

ADUNGO: Arsenal itasalia kuwa timu ya kawaida tu iwapo haitasajili mafowadi matata

August 20th, 2018 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

KWA karibu miaka 14 sasa tangu Arsenal wanyanyue taji la mwisho la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), kikosi hicho bado ni kile kile. Wapinzani wao wakuu wanapozidi kujisuka kila msimu mpya, wao wangali usingizini tu.

Si bure, kikosi hicho kitasalia kuwa kile kile hadi siku ambapo watateremshwa ngazi katika EPL, pengine msimu huu!

Hadi leo, sijaelewa kiini cha Arsenal kutawaliwa na pupa ya kuzitwaa kwa dharura huduma za wachezaji ovyo ambao hawana uwezo wa kuivunia tija ya aina yoyote kila muhula. Sidhani kuna kubwa ambalo mashabiki wa Arsenal wanastahili kutarajia kutoka kwa kikosi chao cha sasa msimu huu iwapo mtindo wao wa usajili na usogora utasalia kuwa ule ule.

Baada ya kupoteza michuano miwili ya ufunguzi wa msimu huu, makosa ya Arsenal yamekuwa ni yale yale na hatimaye wimbo utakuwa ni ule ule wa “subirini mtatuona msimu ujao!” Hivyo ndivyo hali ilivyokuwa wakati wa Wenger, baharia ambaye kwake kufa maji kulikuwa mazoea!

Tangu 2004, Arsenal wamewaaminisha mashabiki wao kwamba ubingwa wa soka ya Uingereza na bara Ulaya si laiki yao. Vipute hivyo si vya ngazi yao na wapinzani wao si wa kufu wala saizi yao. Iwapo sivyo, tazama jedwali la EPL kwa sasa na tupia jicho matokeo yao dhidi ya Man-City na Chelsea katika kipindi cha wiki mbili zilizopita!

Mbona Arsenal isijifunze lolote kutokana na makosa yaliyowagharimu mataji misimu yote hii? Ni kawaida yao. Kwa sasa ni mazoea. Ambalo kocha Unai Emery anatakiwa kukumbushwa siku zote ni kwamba kufanya vizuri katika EPL, kunahitaji kuwa na straika kiongozi wa kuiongoza timu. Timu inaweza kuwa bora kwenye maeneo mengine yote, ikatengeneza nafasi nyingi za kufunga, lakini inapokosa mvamizi mwenye ufundi wa kupachika mabao, madhara yake huwa makubwa na hutikisa kampeni za msimu mzima.

Pili, ufufuo wa Arsenal utategemea jinsi Emery atakavyojishughulisha katika soko lijalo la uhamisho. Katika miaka ya hivi karibuni, Arsenal wamekosa wachezaji wa kujitolea, wenye uwezo wa kukipigania kikosi kwa jino na ukucha ili kuwavunia ushindi.

Safu ya kati ya Arsenal bado inakosa wachezaji wenye sifa za N’Golo Kante (Chelsea), Paul Pogba (Man-United) au Kevin De Bruyne (Man-City). Watatu hao ni miongoni mwa wachezaji wenye nguvu na pumzi zisizokwisha kwa urahisi kila wanapowajibishwa uwanjani. Viungo wote ambao Arsenal wamejinasia tangu kuondoka kwa Vieira wamekuwa na viwango vya kulinganishwa na maji ya baharini tu – yanajaa na wakati mwingine yanakupwa.

Arsenal wanahitaji viungo wawili zaidi ambao watashirikiana vilivyo na Mesut Ozil katika safu ya kati. Ingawa Ozil ni miongoni mwa wachezaji wabunifu zaidi, udhaifu wake ni kwamba yeye si kiongozi.

Arsenal wanahitaji sungura wa soka atakayewaundia Pierre-Emerick Aubameyang na Alexandre Lacazette nafasi za wazi katika safu ya mbele. Sifa hiyo muhimu ndiyo inayokosekana kwa Alex Iwobi, Aaron Ramsey, Henrikh Mkhitaryan na Mohamed Elneny. Ubora wa Ozil ugani hudhihirika kila anapopangwa na wachezaji wazuri ugani. Hilo lilionekana wazi kila alipocheza kwa pamoja na Alexis Sanchez.

kabla ya nyota huyo mzawa wa Chile kutua ugani Old Trafford kuvalia jezi za Man-United msimu jana.