Michezo

ADUNGO: Baada ya kuizima nyota ya Ghana, Harambee Stars sasa wapangiwe mechi nyingi za kujifua

September 10th, 2018 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

HATUA ya Harambee Stars ya kuwabamiza Ghana katika mechi ya pili ya Kundi F mwishoni mwa wiki jana iliweka hai matumaini yao ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) kwa mara ya kwanza mwaka ujao tangu 2004.

Nawapongeza vinara wa Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) kwa kukipangia kikosi cha Stars msururu wa mechi za kupimana nguvu kabla ya kibarua hicho dhidi ya Ghana waliopokea kichapo cha 1-0 uwanjani MISC Kasarani licha ya kikosi cha nyumbani kukamilisha mechi na wachezaji 10 pekee uwanjani. Beki Joash Onyango alionyeshwa kadi nyekundu katika kipindi cha pili.

Kabla ya Stars kushuka dimbani kuvaana na Ghana wikendi iliyopita, vijana hao wa kocha Sebastien Migne walikuwa wamekomolewa na Swaziland waliowapokeza kichapo cha 1-0 mjini Machakos kabla ya kujinyanyua dhidi ya Equatorial Guinea kwa kuwapiga 1-0 kwenye mechi nyingine ya kupimana nguvu.

Baadaye, FKF ilifanikisha mipango ya timu ya taifa ya kusafiri jijini Mumbai, India kushiriki (kwa mwaliko) kipute cha kuwania ubingwa wa Hero Intercontinental. Kivumbi hicho kilichong’oa nanga mnamo Juni 1, 2018, kilishirikisha pia New Zealand, Chinese Taipei na wenyeji India.

Ingawa ipo haja na ulazima wa kuwaratibia Stars mechi za kirafiki dhidi ya mataifa ya bara Ulaya, nahisi kwamba tajriba ya kupepetana na Swaziland, Equatorial Guinea, New Zealand, India na Chinese Taipei ilikuwa jukwaa mwafaka kwa vijana wa Migne kujifunza mengi kutoka kwa wapinzani wao hao.

Ingawa sina uhakika, huenda FKF kwa pamoja na Migne wanawazia kwa sasa kuwakutanisha Stars na vikosi vya haiba kubwa zaidi barani Afrika kufu ya Senegal, Algeria, Cameroon, Nigeria na Ivory Coast.

Itakuwa tija na fahari zaidi kushuhudia Stars siku moja ikipepetana kirafiki na vikosi kama vile Misri, Tunisia na Morocco ambavyo vilinogesha fainali za Kombe la Dunia nchini Urusi mwaka huu.

Itaridhisha sana kuwaona Stars chini ya Migne, wakivaana kirafiki na mataifa kama vile Ufaransa, Croatia, Ujerumani, Brazil, Ubelgiji, Ureno, Argentina, Uhispania, Uingereza, Italia na timu nyinginezo za kufu, laiki na kiwango hicho!

Hatua kubwa za kiasi hicho zitakuwa ithibati za kukomaa kwa kikosi cha Stars kadri inavyopania kuimarisha kampeni zao za kufuzu kwa fainali za AFCON 2019 nchini Cameroon.Sina shaka kwamba Stars wataimarika hata zaidi chini ya Migne.

Kabla ya kushuka dimbani kuvaana na Ghana, Stars wanajivunia historia ya kuwazidi maarifa wapinzani wao hao mara moja pekee, ushindi wa 3-1 waliousajili katika mechi ya kirafiki iliyowakutanisha jijini Accra, Ghana mnamo Juni 13, 2003.

Vikosi hivyo viwili viliwahi kukutana uso kwa macho kwa mara nyingine mnamo Machi 23, 2005 ambapo Kenya iliwalazimishia Ghana sare ya 2-2 jijini Nairobi. Kibarua sasa kwa Kenya ambao kwa pamoja na Ethiopia na Sierra Leone wamepangwa katika Kundi F, ni kusajili matokeo mazuri dhidi ya wapinzani wao hao.

Kenya imewazidi Ethiopia maarifa mara 14 huku wakisalia wanyonge machoni pa wapinzani hao mara 12 na kutoka sare mara tisa. Kenya ilibamizwa na Ethiopia 2-0 ugenini mnamo Juni 21, 2015 na kulazimishiwa sare tasa jijini Nairobi mnamo Julai 4, 2015. Hadi kufikia sasa, Ghana wanajivunia uongozi wa Kundi F baada ya kuwapepeta Ethiopia 5-0 jijini Kumasi nao Sierra Leone wakawakomoa Kenya 2-1 katika mechi za kwanza zilizopigwa mnamo Juni 2017.