Michezo

ADUNGO: Chini ya Klopp, Liverpool inaweza kufanya lolote katika soka ya Uingereza na hata Ulaya nzima

April 9th, 2018 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

INGAWA Manchester City walipigiwa upatu kunyakua jumla ya mataji matatu msimu huu, inaelekea kwamba kikosi hicho cha Pep Guardiola kitalazimika kuridhika na ufalme wa soka ya Uingereza na ubingwa wa League Cup pekee.

Hii ni baada ya Liverpool kudidimiza yake katika soka ya bara Ulaya (UEFA) kwa kichapo cha 3-0 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa robo-fainali za kivumbi hicho wiki iliyopita.

Ingawa Man-City wamekuwa na msimu mzuri ambao umewashuhudia wakicheza mpira wa kuvutia tangu mwanzo wa msimu hadi kufikia sasa, miamba hao wa Uingereza wana nafasi finyu ya kufikia nusu-fainali za UEFA msimu huu.

Ili kuweka hai matumaini ya kuwabwaga Liverpool katika marudiano ya UEFA wiki hii, ilitarajiwa Man-City wangalijituma zaidi na kuwakomoa watani wao Manchester United katika gozi la EPL lililowakutanisha mwishoni mwa wiki jana uwanjani Etihad.

Hata hivyo, utepetevu wa Man-City uliwaruhusu wageni wao kutoka nyuma kwa mabao 2-0 na hatimaye kuwabamiza 3-2 kwenye gozi hilo la kusisimua.

Wanapojiandaa kuwalaki Liverpool kesho, Man-City wana kibarua kigumu cha kujinyanyua baada ya makali yao kuzimwa na Man-United katika mchuano uliokuwa wa pili mfululizo kwa vijana wa Guardiola kupoteza msimu huu.

Kwa kuwalaza Man-City kwa idadi kubwa ya mabao, Liverpool ni mpinzani ambaye kwa sasa amedhihirisha kuwa ana uwezo mkubwa wa kunyanyua ufalme wa UEFA na hastahili kupuuzwa.

Ingawa Man-City iliwadhalilisha Liverpool katika mechi ya EPL mwanzoni mwa msimu huu kwa kichapo cha 5-0 ugani Etihad, kikosi cha kocha Jurgen Klopp kwa sasa ni timu tofauti kabisa. Chini ya mkufunzi huyo wa zamani wa Borussia Dortmund, viwango vya wachezaji wengi wa Liverpool vimeimarika maradufu.

Hili limedhihirishwa kupitia kwa ukali wa nyota Sadio Mane, Alex Oxlade-Chamberlain, Roberto Firmino na Mohamed Salah ambaye anapigiwa upatu kuibuka Mfungaji Bora wa EPL msimu huu. Hadi sasa, Liverpool na Man-United ndizo timu za pekee ambazo zimewashinda Man-City katika kampeni za EPL msimu huu.

 

Mashambulizi ya kutisha 

Silaha kubwa ya Liverpool ni uwezo wao wa kuanzisha mashambulizi ya kushtukiza kupitia kwa wachezaji wao wenye kasi sana na ambao hawahitaji nafasi nyingi ili kufunga mabao. Huu ndio upekee wa kikosi cha Klopp!

Kwa namna moja au nyingine, Liverpool ni timu ambayo ubora wake utadhihirika kila inapocheza na mpinzani aliye na mazoea ya kumiliki mpira kwa muda mrefu na amabye anacheza soka ya kushambulia kama mabingwa watarajiwa wa EPL, Man-City.

Mnamo 2013, Klopp aliwachochea Dortmund kutinga fainali ya UEFA baada ya kuwabandua Real Madrid kwenye nusu-fainali.

Ingawa kulikuwepo na klabu nyingi zenye vikosi bora zaidi kuliko Dortmund wakati huo, mfumo na upekee wa mbinu za ukufunzi wa Klopp uliwatambisha wapambe hao wa soka ya Ujerumani.

Man-City kwa sasa ina kikosi bora zaidi kuliko Liverpool. Hata hivyo, iwapo kuna timu iliyo na nafasi kubwa sana ya kusambaratisha kabisa ndoto za Man-City za kutwaa ubingwa wa UEFA, basi ni Liverpool inayonolewa na Klopp!