Michezo

ADUNGO: Ilivyo, naona ni Liverpool na Man-City, kisha Chelsea na Arsenal katika 4-bora

September 17th, 2018 2 min read

NA CHRIS ADUNGO

LICHA ya Liverpool na Chelsea kuonyesha ishara za ukubwa wa kiu yao katika jitihada za kutawazwa mabingwa wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu, mtandao wa Mirror Football nchini Uingereza bado umewapa Manchester City nafasi kubwa ya kupiku wapinzani wao wakuu kwa muhula wa pili mtawalia.

Chini ya mkufunzi Jurgen Klopp, Liverpool wanapigiwa upatu na Mirror Football kumaliza kivumbi cha EPL msimu huu katika nafasi ya pili huku Chelsea wakiwekwa katika nafasi ya tatu.

Arsenal wanatazamiwa kujinyanyua vilivyo chini ya kocha mpya Unai Emery na kufunga mduara wa nne-bora na hivyo kuwasaza Tottenham na Man-United nje ya kivumbi cha kuwania ufalme wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Hii ni mara ya tatu mfululizo kwa Man-City kupewa nafasi ya kutwaa ubingwa baada ya wachanganuzi wengi wa soka kuwapigia chapuo kutokana na ubora wa rekodi ya kocha Pep Guardiola na kiwango cha sasa cha kikosi chake.

Guardiola anapigiwa upatu kutwaa ubingwa wa taji la EPL msimu huu baada ya kujinasia huduma za kiungo mzawa wa Algeria, Riyad Mahrez aliyeagana na Leicester City. Kwa kujitwalia maarifa ya Mahrez, kocha huyo mzawa wa Uhispania amejivunia ubunifu wa kiwango cha juu kadri safu yake ya kati itakavyopania kushirikiana na wavamizi Sergio Aguero na Gabriel Jesus.

Kwa hakika, itakuwa vigumu sana kwa wapinzani wa Man-City hasa Chelsea na Man-United kuwapiga breki msimu huu wanapoazimia kuwa kikosi cha kwanza baada ya miaka 10 kutetea kwa mafanikio ubingwa wa EPL.

Chelsea hawana kikosi kibaya, ila tofauti na klabu nyinginezo, wameshindwa kabisa kuboresha kikosi chao katika muhula huu. Ingawa kocha Maurizio Sarri alimtwaa Jorginho kutoka Napoli, klabu hiyo ilishindwa kusajili wachezaji wenye uwezo wa kuendeleza mchezo wao na kukiimarisha kikosi kizima hasa katika safu ya uvamizi. Si bure, mwenge wa makali yanayojivuniwa na Chelsea hivi sasa utazimwa hivi karibuni.

Inasalia kwamba, kikosi cha pekee chenye uwezo wa kuvuruga maazimio ya Man-City ni Liverpool. Hili nalisistiza sana kwa sababu chini ya Klopp, viwango vya wachezaji wengi wa Liverpool vimeimarika maradufu; na siri yao kubwa ni uwezo wao wa kuanzisha mashambulizi ya kushtukiza kupitia kwa wachezaji wenye kasi sana na ambao hawahitaji nafasi nyingi ili kufunga mabao.

Liverpool ni timu ambayo ubora wake utadhihirika kila inapocheza na mpinzani aliye na mazoea ya kumiliki mpira kwa muda mrefu na ambaye anacheza soka ya kushambulia kama vile Man-City.

Hapana shaka kwamba Man-City na Liverpool kwa sasa wana vikosi bora zaidi kuliko hata Arsenal ambao chini ya Emery, naona nikiunga mkono utafiti wa Mirror Football kwamba, watatua salama ndani ya mduara wa nne-bora kufikia mwishoni mwa msimu huu.

Hadi kufikia sasa, hakuna kitu kizuri zaidi kuliko kuwa shabiki wa Liverpool. Usajili ambao Klopp tayari aliufanya muhula huu unaashiria ukubwa wa kiu aliyonayo ya kutia kibindoni ufalme wa EPL na taji la UEFA.

Japo matumizi yake ya fedha yalishtumiwa na mahasimu wake wakuu katika EPL, naona kwamba Klopp amepania kujenga kikosi thabiti kitakachohimili mawimbi yaushindani katika EPL na UEFA. Baada ya kujinasia huduma za viungo Naby Keita na Fabinho, Klopp alimsajili fowadi Xherdan Shaqiri kabla ya kujitwalia maarifa ya kipa Alisson Becker ambaye ni mzawa wa Brazil.