Michezo

ADUNGO: Naona makombe yote ya UEFA yakielekea kwa timu za La Liga, Real Madrid na Atletico Madrid

April 30th, 2018 2 min read

Na CHRIS ADUNGO

KATI ya timu nne za mwisho zinazofukuzia ufalme wa soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu, nahisi kwamba ni Real Madrid ndiyo iliyo katika nafasi nzuri zaidi ya kunyanyua taji hilo baada ya kukizamisha chombo cha Bayern Munich kwa 2-1 wiki iliyopita.

Haitakuwa ajabu wala miujiza kuwaona Atletico Madrid pia wakitawazwa mabingwa wa Ligi ya Uropa msimu huu baada ya kikosi hicho kudidimiza matumaini ya Arsenal kwa kusajili sare ya 1-1 katika mchuano wa mkondo wa kwanza wa nusu-fainali iliyopigwa ugani Emirates mnamo Alhamisi iliyopita.

Iwapo kweli vikosi viwili vinavyopiga soka ya Uhispania (La Liga) vitatawala mapambano haya mawili ya bara Ulaya msimu huu, basi hilo ni tukio litakaloturejesha tena katika mjadala wa ni ipi ligi bora zaidi kati ya EPL, Ligue 1, Serie A, La Liga na Bundesliga.

Japo Liverpool wanapigiwa upatu wa kuwabandua AS Roma kwenye nusu-fainali ya UEFA na hatimaye kuyazima makali ya Real ambao dalili zote zinaashiria kwamba watatinga hatua hiyo, nahisi kwamba kibarua kilichopo mbele ya kocha Jurgen Klopp si vivi hivi!

Huku mafanikio haya ya klabu za La Liga yakipania kutusadikisha kwamba soka ya Uhispania ndiyo inayosheheni utajiri mkubwa zaidi wa talanta na vipaji, nasisitiza kuwa ubora wa EPL siku hizi umo tu katika wingi wa fedha zinazomwagwa sokoni kwa minajili ya kusajili wachezaji wapya na upeperushaji wa moja kwa moja wa mechi za kivumbi hicho.

Huku ikiwa vigumu sana kwa mashabiki kutabiri mshindi wa mechi tofauti za EPL, ni rahisi mno kufahamu matokeo ya mechi za Uhispania, hasa kama mapambano hayo yatahusisha timu za Real, Barcelona na Atletico.

Kinachowachochea mashabiki wengi kuamini kwamba La Liga ni bora zaidi kuliko EPL ni ubabe wa watani wakuu wa soka ya Uhispania; yaani Real, Barcelona na Atletico ambao kwa miaka mingi, wametawala La Liga na wameogopewa sana na wapinzani wao katika soka ya bara Ulaya.

Kwa mara nyingine, naona itakuwa vigumu kwa vikosi vya Uingereza (Liverpool na Arsenal) kusajili matokeo bora dhidi ya Real na Atletico katika fainali ya UEFA.

Ingawa Liverpool wamekuwa na msimu mzuri ambao umewashuhudia wakicheza mpira wa kuvutia chini ya kocha Jurgen Klopp, kuvuja kwa safu ya ulinzi ya miamba wa Uhispania kunawapa nafasi finyu ya kuwazidi maarifa Real ambao matumaini yao yote ya kujiepushia aibu msimu huu na kumuokoa mkufunzi Zinedine Zidane, yako katika ulazima wa kunyanyua ufalme wa UEFA.

Sawa na Atletico ambao naona sasa wakivaana na Olympique Marseille kwenye fainali ya Uropa, makali ya Real yameshuka pakubwa katika kampeni za La Liga msimu huu.

Si ajabu kuelewa kiini cha Real kuanza kuhemea mapema maarifa na huduma za nyota Harry Kane, Paul Pogba, David De Gea, Eden Hazard, Mohamed Salah, Thibaut Courtois, Anthony Martial na Dele Alli.