Michezo

Pellegrini na Benitez wananusia shoka EPL licha ya tajriba

September 17th, 2018 2 min read

Na CHRIS ADUNGO 

KOCHA Manuel Pellegrini wa West Ham United amekiri kwamba kiwango cha utepetevu kambini mwa kikosi chake ni cha kutisha na huenda waajiri wake wakateremshwa ngazi mwishoni mwa kampeni za Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) msimu huu iwapo hawatajinyanyua mapema mkiani mwa jedwali.

Kwa mujibu wa kocha huyo mzawa wa Chile, West Ham wamevaliwa na hofu kuhusu kiwango cha kusuasua kwao chini ya kocha mwenye uzoefu mkubwa na tajriba pana.

Katika michuano minne ya ufunguzi wa kampeni za EPL msimu huu, vijana wa Pellgerini ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Man-City, walikomolewa 4-0 na Liverpool kabla ya Bournemouth kuwabamiza 2-1. Baadaye walipepetwa 3-1 na Arsenal kabla ya limbukeni Wolves kuwaliza 1-0. Mbali na kuwaning’iniza West Ham pembamba mkiani mwa jedwali, matokeo hayo yanakiweka chuma cha Pellegrini motoni na huenda wakati wake wa kuhudumu kambini mwa kikoi hicho ukakatika wakati wowote.

Mwanzo duni wa West Ham United katika kampeni za EPL msimu huu unarejesha kumbukumbu za 2010-11 ambapo walishushwa daraja mwishoni mwa muhula huo baada ya kupoteza mechi zao nne za ufunguzi wa ligi.

Pellegrini na mwenzake Rafael Benitez wa Newcastle United ni wakufunzi wawili ambao walikuwa wamezoea maisha ya hadhi ya juu katika vikosi vyao vya awali.

Lakini kwa sasa wamejipata mkiani mwa Ligi Kuu huku klabu zao zikiwemo ndani ya mduara wa timu tatu za mwisho.

Chini ya Benitez, Newcastle United wamepoteza michuano minne na kutoka sare mara moja katika michuano mitano ya ufunguzi wa EPL msimu huu, hali ambayo huenda ikawaweka waajiri wake katika ulazima wa kufikiria upya kumhusu.

Baada ya kulazwa 2-1 na Tottenham Hotspur katika mechi ya kwanza, vijana wa Benitez waliambulia sare tasa dhidi ya limbukeni Cardiff City kisha wakapoteza 2-1 walipokutana na Chelsea.

Walipokezwa kichapo cha 2-1 na mabingwa watetezi Manchester City kabla ya kupokea kichapo sawa na hicho walipokutana na Arsenal wikendi jana.

Katika matukio ya awali yanayodhihirisha ukubwa wa kiwango na haiba ya Benitez, kocha huyo mzawa wa Uhispania anajivunia kutwaa taji la Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) akiwa na Liverpool mnamo 2005.

Pia amekusanya vikombe vya Ulaya akidhibiti mikoba ya Valencia na Chelsea huku naye Pellegrini akishinda ubingwa wa EPL akidhibiti usukani wa Man-City.

Newcastle kwa kiasi fulani wamepondwa na ratiba yao. Kikosi hicho kimekuwa na wakati mgumu katika mechi za nyumbani baada ya kupangwa dhidi ya Tottenham na Chelsea kisha Man-City kwa usanjari huo. Wakati wa pekee ambapo vijana wa Benitez wangenusia ushindi ni walipopata mkwaju wa penalti dhidi ya Cardiff katika dakika ya 96 ila kiungo Kenedy akapoteza.

Tatizo la Benitez ni ukosefu wa mabao katika safu yake ya mbele. Licha ya kujinasia huduma za mvamizi Salomon Randon kutoka West Bromwich Albion msimu huu, Newcastle United wamefunga mabao manne pekee kutokana na mechi tano zilizopita.

Kwa upande wa West Ham Utd, wanaokoselewa zaidi ni wachezaji kama vile Jack Wilshere na Mark Noble ambao hawana nguvu za kutimiza mbinu za kushambulia za Pellegrini au kukabiliana vilivyo na wapinzani wao.

West Ham walionyesha tumaini la kujinyanyua walipocheza na Arsenal licha ya kushindwa. Ingawa ushindi wao wa 3-1 dhidi ya AFC Wimbledon ulitarajiwa kuwa mwamko mpya kambini mwao, kikosi hicho kilizidiwa maarifa na Wolves katika mchuano uliofuata.