Habari Mseto

Afa kwa kujirusha baharini toka ferini

November 25th, 2019 1 min read

Na Mohamed Ahmed

MWANAMUME mmoja alifariki Jumapili baada ya kujirusha kutoka kwenye feri katika kivuko cha Likoni.

Jamaa huyo asiyejulikana alijirusha kutoka kwenye feri ya Mv Harambee muda wa saa saba na nusu usiku, wakati feri hiyo ilipokuwa inaelekea Mombasa kisiwani kutoka eneo la Likoni.

Shirika la Huduma za Feri (KFS) lilisema katika taarifa kuwa jamaa huyo alionekana kutokuwa katika fahamu zake vyema.

“Jamaa huyo ambaye alikuwa amevalia fulana nyeupe na suruali nyeusi alitoka mahali alipokuwa amekaa na kujirusha majini,” inasema taarifa yao.Kulingana na ripoti ya polisi iliyoonwa na Taifa Leo, jamaa huyo alijirusha feri ikiwa imefika katikati ya bahari.

KFS ilisema kuwa baada ya tukio hilo maafisa wake walifika mahali hapo lakini kwa sababu ya mawimbi na giza hawakuweza kumuokoa jamaa huyo.