Habari Mseto

Afariki akisema kuongezwa damu ni kinyume na imani yake

January 14th, 2019 1 min read

NA NICHOLAS KOMU

MGONJWA mmoja mnamo Jumamosi alifariki katika Hospitali ya Rufaa ya Nyeri baada ya kukataa kuongezewa damu mwilini akisema ni kinyume cha imani yake ya kidini.

Samuel Maina alifariki kutokana na matatizo ya figo baada ya kukataa kuwekwa damu, uamuzi uliozua mgawanyiko mkubwa katika familia yake.

Stakabadhi zilizoonekana na Taifa Leo zilionyesha kwamba mgonjwa huyo alipaswa kuoshwa figo lakini alihitajika kuongezewa damu kwanza kabla ya huduma hiyo.

Gathuku Gachini, nduguye marehemu, alisema kwamba madaktari hospitalini humo walishauri kwamba kwa kuwa Bw Maina alikuwa na kiwango cha chini cha damu, alihitaji kuongezewa.

Hata hivyo, mambo yalichukua mwelekeo tata marehemu alipokataa ushauri huo kwa msingi kwamba imani yake ya kidini inakataza muumini kuongezewa damu.

Mhandisi huyo mstaafu ni muumini wa kanisa la Jehova Witness ambalo itikadi na mafundisho yake huharamisha muumini kuongezewa ama kutoa damu yake.

Waumini wa kanisa hilo hudai kwamba Bibilia huharamisha kuongezwa damu, hii ikiwa ni tofauti na dini nyingine za Kikristo zinazozingatia uhai wa binadamu kama kitu muhimu sana.

Ingawa baadhi ya watoto wake na wanafamilia walisimama kidete na kuusifu uamuzi wa mwendazake, mkewe pamoja na watoto wake wengine waliupinga.

Maji yalipozidi unga na mgonjwa huyo kushikilia msimamo wake, madaktari baada ya kukosa kumshawishi hawakuwa na jingine ila kumpa stakabadhi ili azitie saini kuonyesha kwamba alikataa kuongezewa damu mwilini.

Hata hivyo, jitihada zaidi za marafiki na baadhi ya wanafamilia kumtaka abadili msimamo wake ziliangukia sikio la kufa na akaaga.