Michezo

AFC Leopards pabaya katika CAF baada ya kukubali sare

February 12th, 2018 2 min read

Duncan Otieno (kulia) wa AFC Leopards apambana na Piepre Michael Tavina Rakotorisoa wa Fosa Junior ya Bukini kwenye mechi ya Mashirikisho ya CAF uwanjani Bukhungu, Kakamega Jumapili. Picha/Isaac Wale

Na GEOFFREY ANENE

Kwa Muhtasari:

  • Ingwe yakabwa koo 1-1 na Fosa Juniors uwanjani Bukhungu
  • Mechi ilibadilika pale Fosa iliposawazisha dakika ya 16.
  • Fosa inashiriki mashindano ya Afrika kwa mara ya kwanza kabisa.

AFC Leopards ilihatarisha kampeni yake ya kusonga mbele kwenye mashindano ya Afrika ya Confederations Cup baada ya kukabwa koo 1-1 na Fosa Juniors uwanjani Bukhungu mjini Kakamega, Jumapili.

Vijana wa kocha Robert Matano, ambao waliona lango kupitia chipukizi Yusuf Mainge, lazima wapige Fosa kwa angaa 1-0 au sare ya angaa 2-2 katika marudiano nchini Madagascar ili wasalie mashindanoni.

Fosa itahitaji sare tasa pekee nyumbani ili kubandua Ingwe nje. Penalti zitaamua timu itakayoingia raundi ya kwanza ikiwa Leopards italazimisha sare ya 1-1 katika mechi ya marudiano.

 

Dakika ya 3

Mainge, ambaye alinyakuliwa kutoka Green Commandoes ya Shule ya Upili ya Kakamega, aliipa Leopards matumaini. Aliamsha maelfu ya mashabiki katika uwanja huo unaobeba mashabiki 20, 000 dakika ya tatu. Hata hivyo, mkondo wa mechi ulibadilika pale Fosa iliposawazisha dakika ya 16.

Fosa ilipata nafasi kadhaa nzuri za kuimarisha magoli yake katika dakika 45 za kwanza, lakini haikuzitumia vyema.

Leopards, ambayo imekuwa ikikumbwa na matatizo ya kifedha tangu wadhamini wake wakuu kampuni ya bahati-nasibu ya SportPesa itangaze kuondoa usaidizi wake Januari 1, 2018, inatarajiwa kuzuru kisiwa cha Madagascar hapo Februari 21 kwa mchuano wa marudiano.

Mabingwa hawa wa zamani wa Ligi Kuu ya Kenya wamerejea katika mashindano ya Afrika baada ya kuwa mashabiki kwa misimu mitatu mfululizo.

 

Matumaini

Fosa inashiriki mashindano ya Afrika kwa mara ya kwanza kabisa. Kabla ya kukutana na Fosa, Leopards ilikuwa imewapa mashabiki wake matumaini ya kufanya vyema katika Confederations Cup.

Ilipepeta mabingwa mara 26 wa Sudan, Al Hilal, 4-2 na kulemea miamba wa Uganda, Kampala Capital City Authority 2-1 humu nchini.
Katika mashindano haya ya daraja ya pili ya Afrika, timu ya Cape Town City kutoka Afrika Kusini iliyoajiri mfungaji bora wa Ligi Kuu ya

Kenya ya mwaka 2017, Masoud Juma, ilianza vyema kampeni yake ya Confederations Cup, Jumamosi.

Vijana wa kocha Benni McCarthy walilemea wenyeji wao Young Buffaloes ya Swaziland 1-0 kupitia bao la Mghana Nana Akosah-Bempah. Juma hakushiriki mchuano huu kutokana na jeraha.