Michezo

AFC Leopards yaendelea kusajili msururu wa matokeo mabaya

February 23rd, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

AFC Leopards SC haina mahali pa kujificha baada ya kupokezwa kichapo chake cha sita mfululizo kwa kulimwa 2-0 na Mathare United mnamo Jumamosi na kusalia mbioni kutemwa kutoka Ligi Kuu.

Vijana wa Casa Mbungo waliingia mchuano huu wakiuguza vichapo kutoka kwa Ulinzi Stars 1-0, Gor Mahia 2-0, Mount Kenya United 2-1, Bandari 4-1 na Zoo Kericho 1-0.

Leopards almaarufu Ingwe ilivumilia mashambulizi makali kabla ya kusalimu amri kupitia mabao ya wachezaji wa akiba Ronald Reagan na Tyson Otieno katika dakika za 86 na 92 uwanjani Kenyatta mjini Machakos, mtawalia.

Otieno aliingia katika nafasi ya Kevin Kimani dakika ya 75 naye Reagan alijaza nafasi ya Chris Ochieng’ dakika ya 60.

Dennis Shikayi wa AFC Leopards akiwa na mpira Februari 9, 2019, wakati wa mechi ya Mashemeji ugani Kasarani Gor Mahia iliposhinda Ingwe 2-0. Picha/ Sila Kiplagat

Baada ya kuambulia alama 10 kutokana na ushindi mbili, sare nne na vichapo vinane, Leopards inasalia katika mduara hatari wa kutemwa katika nafasi ya 17, alama moja mbele ya wavuta-mkia Mount Kenya United.

Katika matokeo mengine, Bandari ilikwamilia juu ya jedwali baada ya kulipua Nzoia Sugar 1-0 kupitia penalti safi kutoka kwa Felly Mulumba, Kakamega Homeboyz ilitoka 2-2 dhidi ya mabingwa wa mwaka 2009 Sofapaka uwanjani Bukhungu, Posta Rangers iliridhika na alama moja katika sare ya 1-1 dhidi ya Ulinzi Stars mjini Machakos nayo Chemelil Sugar ikalazimishiwa sare ya 1-1 nyumbani dhidi ya KCB.

Ratiba (Saa tisa alasiri Jumapili): Mount Kenya United na Zoo, SoNy Sugar na Western Stima, Vihiga United na Kariobangi Sharks.