Habari Mseto

AFC yashirikiana na UN Women kuhamasisha wanawake wanaofanya kilimo

November 20th, 2020 2 min read

Na DIANA MUTHEU

SHIRIKA la Mikopo na Ustawishaji Kilimo (AFC) likishirikiana na Kitengo cha Wanawake cha Umoja wa Mataifa (UN Women), limeanza mradi wa kuwahamasisha wanawake wanaofanya kilimo au kilimo-biashara kuhusu jinsi wanavyoweza kupata mikopo au ufadhili ili kuinua halo zao za kiuchumi.

Kulingana na AFC, wanawake wengi nchini wanajihusisha na ukulima lakini wanaopata msaada wa kifedha ni chini ya asilimia 15.

Akizungumza na waandishi wa habari katika hoteli ya Sarova Whitesands mnamo Ijumaa baada ya mkutano na wakulima, haswa wanawake ambapo walizungumzia jinsi wanaweza kupata fedha za kuendeleza kilimo chao na solo ya bidhaa zao, Msimamizi wa kitengo cha mikopo katika shirika la AFC, Bw Bonano Badia alisema kuwa wanalenga kuhakikisha kuwa asilimia 40 ya kina mama wanapata pesa hizo.

“Tuko katika harakati ya kuhakikisha kuwa kuna mikakati maalum ya kutoa fedha kwa wanawake wanaofanya kilimo au kilimo-biashara,” akasema Bw Badia.

Msimamizi wa kitengo cha mikopo katika Shirika la Fedha za Kilimo, (AFC) Bw Bonano Badia akizungumza na waandishi wa habari. Alisema AFC inalenga kuhakikisha asilimia 40 ya wanawake katika sekta hiyo wanapeta fedha za kujiendeleza. Picha/ Diana Mutheu

Bw Badia alisema kuwa baadhi ya sababu ambazo zimepelekea wanawake wengi katika sekta hii kukosa fedha hizo ni kama vile: wanaume kupewa kipaumbele na pia mila na desturi zetu kama Waafrika kuhusu umiliki wa ardhi.

“Tunataka kubadilisha hayo yote polepole na kwa njia ambayo wanawake wataweza kuendelea kupata pesa za kuendeleza kilimo chao. Pia, tutazidi kuelimisha jamii kuhusu umuhimu wa kuwapa wanawake uhuru wa kujiendeleza kupitia kilimo na kilimo-biashara,” akasema huku akiwashauri wasio na uwezo wa kujisimamia wenuewe wajiunge katika makundi ili waweze kufaidika na fedha hizo.

Afisa wa miradi wa UN Women, Bw David Mugo alisema kuwa wanawake wengi katika sekta ya kilimo ni vibarua tu kwa sababu hawana fedha za kutosha kukuza mimea yao wenyewe.

“Zaidi, wengi hawana maarifa kuhusu kilimo cha kisasa. Hata hivyo tumeanza kutoa mafunzo kwa makundi kadhaa katika baadhi ya kaunti nchini,” akasema Bw Mugo huku akiongeza kuwa wametoa mafunzo kwa wakulima 1,800 humu nchini, ambapo wanawake walikuwa 800.

Zaidi alisema kuwa jumla ya Sh130 milioni zilitolewa kwa wakulima hao.

Mkulima mmoja, Rosemary Chege ambaye alifaidika na fedha kutoka shirika la AFC kuendeleza kilimo chake cha kuku aliwasihi wanawake wenzake wajitokeze ili wafaidi na mradi huo.

Rosemary Chege ambaye ni mkulima wa kuku akizungumza na waandishi wa habari. Aliwaomba wanawake wenzake wafike katika vituo vya AFC ili kilimo chao na kilimo-biashara zao zipigwe jeki. Picha/ Diana Mutheu

“Ningependa wanawake wenzangu wafike katika kituo cha AFC kilichoko karibu nao ili kilimo chao na hata biashara zao ziweze kupigwa jeki,” akasema Bi Chege.