Michezo

AFC yawakia Gor kuhusu usajili wa Makwatta

September 5th, 2019 1 min read

Na CECIL ODONGO

MWENYEKITI wa AFC Leopards, Dan Shikanda amechemkia usimamizi wa Gor Mahia kuhusu zogo lililozingira usajili wa mshambulizi John Mark Makwatta ambaye karibu ajiunge na K’Ogalo kabla ya kubadili uamuzi dakika za mwisho Jumatatu.

Shikanda amesema Gor waliwapokonya huduma za kiungo mbunifu Cliftone Miheso ambaye alikuwa amekamilisha mchakato wote wa kujiunga nao kabla ya dirisha la uhamisho kufungwa.

“Gor hawafai kulia kwamba tumetwaa huduma za Makwatta ilhali walitupokonya Miheso mdomoni. Tulikuwa tumekamilisha maswala yote yanayohusiana na usajili wa Miheso lakini ghafla bin vuu akatutoroka baada ya kushawishiwa kujiunga na Gor,” akasema Shikanda kwenye mahojiano na Taifa Leo.

Ingawa alisema usajili wa wachezaji hao haufai kuzua uhasama kati ya klabu hizo mbili, Shikanda alisisitiza kuwa Ingwe ipo kiwango sawa na Gor Mahia na inastahili kujitwalia huduma za wachezaji wa haiba kama tu wapinzani wao.

“Tulimsajili Makwatta baada yake kuvutiwa na ofa tuliyompa na ikilinganishwa na ile ya Gor Mahia. Kwa nini Gor wanafikiri tu kwamba wao ndio wanafaa kuwasajili wachezaji bora? Gor wanafaa kuridhika na sajili walizofanya na kuangazia msimu mpya badala ya kuona walichezewa shere,” akaongeza Shikanda.

Uwezo wa kiuchumi

Afisa huyo alishikilia kwamba wana uwezo wa kiuchumi wa kugharimia mishahara ya Makwatta, akiahidi kwamba makali yake yatadhihirika kwenye mechi atakazosakatia Ingwe kuanzia wikendi ijayo.

“Tulifaulu kuwasajili wachezaji wote tuliowahitaji isipokuwa Miheso. Nimefurahi kwamba wachezaji wetu wapya wameanza kung’aa kwenye vipindi vya mazoezi na tuna matarajio makuu kutoka kwao msimu huu,” akasema.

Kwa upande wake, Afisa Mkuu Mtendaji wa K’Ogalo Omondi Aduda alishauri Ingwe wajitayarishe kwa makabiliano makali uwanjani badala ya kurusha cheche za maneno na kujipiga kifua kwa kumsajili Makwatta.