Michezo

AFCON 2019: Kenya si kali kuliko Tanzania – Amunike

June 27th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KATI ya timu ya Harambee Stars na Taifa Stars gani kali?

Hili ndilo swali kambi za Kenya na Tanzania zinajiuliza, huku zikitaribiwa kumenyana katika mechi ya kufa-kupona ya Kundi C kwenye Kombe la Afrika (AFCON) jijini Cairo nchini Misri mnamo Juni 27, 2019.

Mshambuliaji Michael Olunga ametabiri mechi hiyo yao ya pili itakuwa ngumu.

“Tanzania ni majirani zetu. Itakuwa mechi ngumu. Sisi sote tulipoteza mechi ya ufunguzi. Hakuna matokeo mengine tunataka kutoka kwenye mechi hii isipokuwa alama tatu. Tumejifunza kutokana na makosa tuliyofanya dhidi ya Algeria na tutarekebisha dhidi ya Tanzania,” tegemeo huyo wa Kenya amesema Jumatano.

Mfaransa Sebastien Migne ameshauri vijana wake wa Harambee Stars kuonyesha ukatili wao katika mechi ijayo ambayo ni dhidi ya Tanzania.

“Naamini katika timu yangu na talanta iliyo nayo,” aliongeza.

Kocha wa Tanzania, Emmanuel Amunike amesema anafahamu umuhimu wa mechi hiyo.

“Lazima tushinde mechi hiyo ili matumaini yetu ya kusonga mbele yasalie hai,” amesema Amunike.

Mechi dhidi ya Senegal ilikuwa funzo muhimu sana kwetu.

Kenya si kama Senegal ama Algeria kwa hivyo tuna uwezo wa kupata kitu kizuri kutoka mechi hiyo. Ni kweli, Kenya pia ni wapinzani wakali, lakini tumejiandaa vyema kutwaa pointi tatu kutoka kwao. Sidhani kama Kenya wako bora kutuliko,” raia huyo wa Nigeria amesema.

Kiungo Himid Mao ameshauri Taifa Stars imakinike zaidi na kujitolea kwa dhati dhidi ya Kenya.

Ameongeza, “Tunajua mpira wa Kenya. Tunataka alama zote tatu kutoka kwa mechi hiyo.”

Algeria na Senegal, ambazo pia zitakutana Juni 27, zinaongoza kundi hili kwa alama tatu kila mmoja baada ya kupepeta Kenya na Tanzania kwa mabao 2-0 kila mmoja, mtawalia.

Kenya na Tanzania, ambazo zinarejea katika AFCON baada ya kuwa nje miaka 15 na 39 mtawalia, zitashuka uwanjani 30 June zikitafuta alama zao za kwanza kabisa.

VIKOSI:

Kenya

Makipa – Patrick Matasi, John Oyemba, Faruk Shikalo.

Mabeki – Philemon Otieno, Abud Omar, Bernard Ochieng, Musa Mohammed, Joash Onyango, Joseph Okumu, David Owino, Eric Ouma;

Viungo – Victor Wanyama, Dennis Odhiambo, Erick Johanna, Ayub Timbe, Francis Kahata, Ismael Gonzalez, Ovella Ochieng’, Paul Were, Johanna Omollo;

Washambuliaji – Masoud Juma, Michael Olunga na John Avire.

Tanzania

Makipa – Aishi Manula, Metacha Mhata, Aron Kalambo.

Mabeki – Hassan Ramadan, Vincent Phillipo, Gadiel Michael, Ally Mtoni, Mohammed Hussein, Kelvin Yondani, Erasto Nyoni, Agrey Moris;

Viungo – Feisal Salum, Himid Mao, Mudathir Yahya, Frank Domayo, Farid Mussa, Yahya Zayd;

Washambulaiji – Rashid Mandawa, Mbwana Samatta, Thomas Ulimwengu, John Bocco, Abdillanie Mussa na Simon Msuva.