Michezo

AFCON 2019: Nigeria na Misri zafuzu mapema

June 28th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

CAIRO, Misri

NIGERIA na wenyeji Misri zilikuwa timu za kwanza kufuzu kwa hatua ya 16 Bora ya AFCON baada ya kuandikisha ushindi wa pili mfululizo.

Misri ambao awali waliandikisha ushindi wa 1-0 dhidi ya Zimbabwe waliikung’uta DR Congo kwa 2-0, mabao yaliyopatikana kupitia kwa Ahmed Elmohamady wa Aston Villa na Mohamed Salah wa Livperpool.

Nao Nigeria ambao walianza kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Burundi wakijipatia ushindi wa pili wa 1-0 dhidi ya Guinea, mfungaji akiwa Kenneth Omeruo, zamani mlinzi wa klabu ya Chelsea ya ligi kuu ya EPL, nchini Uingereza.

Uganda na Zimbabwe zilitoka sare ya 1-1 katika mechi ya kundi A la kinyang’anyiro hicho cha Kombe la Mataifa ya Afrika kinachoendelea nchini hapa.

Uganda ilichukua uongozi wa mapema kupitia Emmanuel Okwi baada ya mlinda lango wa Zimbabwe George Chigova kupangua shambulio la Lumala Abdi.

Lakini Zimbabwe ilisawazisha wakati Khama Billiat alipofunga baada ya kazi nzuri katika wingi ya kushoto iliyofanywa na mchezaji Ovidy Karuru.

Mbali na kufunga bao moja, Salah alitoa pasi iliyosababisha kufungwa kwa bao la pili.

Salah alifunga bao lake kwa ujasiri mkubwa hata baada ya kuzungukwa na wachezaji wawili wa DR Congo baada ya mshambuliaji Trezeguet kumuandalia pasi nzuri.

Wakati huohuo mchezaji wa Zimbabwe Knowledge Musona na mchezaji wa Uganda Patrick Kadu wote walikosa fursa nzuri ya kufunga goli.

Musona aligonga mwamba wa goli wakati aliposalia maguu manne na goli baada ya shambulizi la mchezaji wa Zimbabwe Evans Rusike kuokolewa lilipokuwa likikaribia mstari wa goli, Kaddu aliupiga mpira huo nje.

‘Mambo magumu kidogo’

Zimbabwe ambao walikuwa wanalenga kupata ushindi wao wa tatu katika michuano ya AFCON sasa watalazimika kuishinda DR Congo katika mechi yao ya mwisho ya kundi lao, Jumapili ili kuweza kupata nafasi ya kufuzu katika raundi ya muondoano kwa mara ya kwanza.

Mara tu baada ya kujipatia tiketi ya kucheza katika hatua ya 16 Bora, Shirikisho la Soka Nigeria (NFF) limetangaza kuwapa wachezaji hao marupurupu yao, ambapo kila mmoja atapokea Sh1 milioni.

Msemaji wa shirikisho hilo, Ademola Alajire alisema wachezaji hao watapokea pesa hizo leo, kabla ya kucheza mechi ya mwisho Jumapili dhidi ya Madagascar.

Wachezaji hao walikuwa wakipanga kufanya mgomo na hata kutocheza na Guinea. Timu ya wanawake ambayo iliwakilisha taifa hilo kwenye fainali za Kombe la Dunia zinazoendelea nchini Ufaransa pia ilifanya mgomo baada ya malipo yao kucheleweshwa.

Super Eagles inachezea mechi zake mjini Alexandria huku ikilenga kuongoza kundi B baada ya kushinda mechi mbili, huku ikisalia moja.