Michezo

Afcon 2023: Makocha wa timu zilizozembea wafukuzwa kazi

January 26th, 2024 3 min read

NA LABAAN SHABAAN

HATA kabla ya mkondo wa 16 wa Kombe la Taifa Bingwa Afrika 2023 (Afcon) kuanza, wakufunzi sita tayari wamepoteza kazi.

Ni tukio la kushangaza hali hii ikilinganishwa na makala mengine ambapo makocha hususan huondoka baada ya kukamilika kwa kinyang’anyiro.

Makocha kutakiwa kufana katika michuano hii ni ishara kuwa hali ya mchezo wa mpira wa miguu Afrika iko katika hatua za kustawi.

Makocha wa Ghana, Ivory Coast, Algeria, Tanzania, Gambia na Tunisia wamepigwa kalamu baadhi yao wakijiuzulu sababu ya matokeo duni.

Chris Hughton

Kocha wa Ghana, Chris Hughton, raia wa Uingereza, alitimuliwa baada ya Black Stars kuonyeshwa mlango katika makala mawili mtawalia Afcon (2021 na 2023) awamu ya makundi.

The Black Stars walinyukwa na Cape Verde mabao 2-1 katika mechi ya ufunguzi nchini Ivory Coast na kutoka droo na Misri na Msumbiji.

Vijana wa Hughton waliondolewa kufuatia matokeo ya michezo mingine.

Hughton ni kocha wa zamani wa Newcastle, Brighton, na Nottingham Forest ambazo ni klabu za hadhi ya juu katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Domo la kocha Amrouche lamponza

Shirikisho la Kambumbu Tanzania (TFF) lilimuadhibu Adel Amrouche, raia wa Algeria, baada ya kupigwa marufuku mechi nane na kutozwa faini ya Sh1.6 na Shirikisho la Kandanda Afrika (CAF).

Hii ilijiri sababu ya malalamishi ya Shirikisho la Morocco (RMFF) kwa CAF kuhusu matamshi yake kwamba mashirikisho haya yalikuwa yanakula njama kupanga mechi kwa faida ya Morocco.

Kocha Msaidizi Hemedi Suleiman, raia wa Tanzania, alichukua mikoba ya uongozi wa Taifa Stars ambao wameaga mashindano.

Jean-Louis Gasset alitimuliwa, wenyeji wana bahati kuendelea mkondo wa 16

Kocha wa Cote d’Ivoire, Mfaransa, Jean-Louis Gasset, alitimuliwa Januari 24, 2024 baada ya shinikizo kutoka kwa mashabiki na viongozi.

Ilikuwa siku mbili baada ya wenyeji kuaibishwa na Equatorial Guinea mabao 4-0.

Nafasi yake imechukuliwa na mchezaji wa zamani Emerse Fae.

Fae ataongoza Cote d’Ivoire kutafuta ushindi katika mkondo wa 16 watakapochuana na Senegal mnamo Januari 29, 2024.

Jalel Kadri aomba msamaha

Meneja wa Tunisia Jalel Kadri alifutwa kazi baada ya timu yake kumaliza wa mwisho katika Kundi E.

“Kwa heshima ya wananchi wa Tunisia, tunaomba msamaha kwa matokeo haya,” alisema Jalel ambaye ni kocha mzaliwa wa Tunisia anayechunguzwa kwa madai ya ufisadi hasa kufungamana na kukosa stakabadhi za kitaaluma kuwa meneja wa mchezo wa mpira wa miguu.

Miamba hawa wa Afrika walihitajiwa kupiga Afrika Kusini ili kuendelea na kinyang’anyiro lakini walitoka sare tasa Januari 24, 2024.

Wenzao wa kundi E – Mali, Afrika Kusini na Namibia – walifuzu kuingia hatua ya kuondoana.

Jalel aliongoza Tunisia katika Kombe la Dunia waliposhangaza dunia kwa kushinda Bingwa mtetezi Ufaransa 1 – 0 ila ushindi huu haukuwasaidia kufuzu hatua ya mtoano.

Mzawa huyu wa Tunisia angeendelea na ukocha kama wangefuzu raondi ya 16 sababu lilikuwa hitaji lake yeye kurefushiwa mkataba na Shirikisho la Kandanda Tunisia.

Gambia yapoteza mechi zote

Kocha wa timu ya taifa ya Gambia, Tom Saintfiet, raia wa Ubelgiji, alijiuzulu baada ya kushindwa kuingiza kikosi hicho hatua ya 16 bora makala ya Afcon 2023 inayorindimwa nchini Cote d’Ivoire.

Hatua hiyo ilisababishwa na kipigo cha mabao 2-3 dhidi ya Cameroon katika awamu ya makundi mnamo Jumanne Januari 23, 2024.

Gambia iliibuka mkia katika Kundi C baada kutovuna alama yoyote wakilimwa na Senegal, Guinea na Cameroon.

Sawa na Tunisia, Algeria, mabingwa wa Afcon 2019, pia walimaliza mwisho katika kundi lao.

Kocha wa Algeria Djamel Belmadi alibwaga zana za kazi baada ya kuchakazwa na Mauritania 1-0.

Belmadi, mzaliwa wa Paris lakini raia wa Algeria, alikuwa nahodha wa Algeria katika makala ya Afcon 2004, na alijukumika nafasi ya ukocha Algeria iliposhinda kombe hili 2019 nchini Misri.

Rais wa Shirikisho la Kandanda Algeria Walid Sadi alisema kuwa waliafikiana na Belmadi kutengana kikazi.

“Tunamshukuru Djamel kwa kila kitu alifanyia timu hii na tunamtakia kheri akiendelea na taaluma hii,” alisema Sadi.

Miaka ya hivi karibuni kumekuwa na shinikizo kwa mataifa ya bara afrika kushirikisha makocha wa nyumbani kukuza kandanda badala ya utegemezi wa wakufunzi wa mataifa ya kigeni hasaa kutoka Bara la Ulaya.

Hali hii ilikuwa bayana hivi karibuni zaidi katika Kombe la Dunia Morocco walipofika awamu ya nusu fainali 2022 wakiongozwa na kocha wa nyumbani Walid Regragui.

Senegal, ambao ni mabingwa watetezi wa Afcon, wananolewa na Msenegali Aliou Cisse ambaya alikuwa mchezaji awali.

Kadhalika, Cameroon waliotinga mkondo wa 16, wanafunzwa na mchezaji wao wa zamani Rigobert Song.

Timu ya taifa ya Mali pia imejitoma ndani ya timu 16 bora ikiongozwa na mchezaji wao wa zamani Eric Sekou Chelle katika wadhifa wa kocha.

Wataalamu wa michezo wanasema uhusishaji wachezaji wa zamani ama makocha wa nyumbani ni hatua za kwanza kustawisha kambumbu ya Afrika.