AFCON: Atawika nani kati ya Olunga na Mo’ Salah?

AFCON: Atawika nani kati ya Olunga na Mo’ Salah?

Na CECIL ODONGO

HUKU timu ya taifa Harambee Stars ikitarajiwa kumenyana na Misri katika mechi ya kufuzu Taifa Bingwa Afrika (AFCON) Alhamisi, mashabiki wanasubiri kuona nani mkali kati ya mshambuliaji matata Michael Olunga na nyota wa Liverpool, Mohammed Salah.

Kikosi cha Misri kinachoshirikisha Salah (kushoto pichani) na Mohamed Elneny wa Arsenal, kimewasili nchini tayari kwa ngarambe hiyo itakayosakatwa uwanjani Kasarani kuanzia saa moja jioni.

Salah amekuwa moto wa kuotea mbali msimu huu na ingawa fomu ya Liverpool imekuwa mbovu katika mechi za hivi karibuni, ndiye anaongoza chati ya ufungaji katika Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa mabao 17.

Kwa upande wake, Olunga pia amekuwa akicheka na nyavu kwa raha zake tangu ajiunge na Al Duhail ya Qatar mnamo Januari, kutokea Kashiwa Reysol ya Japan.

Olunga, 27 ameshatingia timu yake mpya mabao saba baada ya kucheza mara 12.

Hapo jana, kocha Jacob ‘Ghost’ Mulee alimpa Olunga unahodha kutokana na kutokwepo kwa kiungo wa Montreal Impact Victor Wanyama.

Mwanadimba huyo alisema kuwa jukumu lake kuu ni kusaidia Harambee Stars kuibwaga The Pharaos, japo Stars ina nafasi finyu ya kufuzu makala ya Afcon itakayoandaliwa mnamo Juni, 2022 -nchini Cameroon.

Olunga alikosa mechi mbili za Stars zilizopita dhidi ya Kisiwa cha Comoros ambapo walisajili sara ya 1-1 nyumbani Novemba 11 2020 na kupoteza 2-1 ugenini Novemba 15.

“Mechi yoyote ya timu ya taifa huja na presha hasa wakati huu ambapo sasa nimepokezwa mikoba ya unahodha. Hata hivyo, nina wingu la matumaini kwamba tutashinda kwa sababu kila mchezaji amedhihirisha uweledi wake mazoezini,” akasema Olunga jana baada ya hafla ya chamcha iliyoandaliwa na FKF kwa ushirikiano na wafadhili wao Odi bets jijini Nairobi.

Mulee hata hivyo alitangaza kwamba mshambulizi wa Kariobangi Sharks Eric Kapaito ambaye anaongoza chati ya ufungaji kwenye ligi kuu amepata jeraha na hatakuwa kikosini.

Mlinzi wa Elsfborg ya Sweden Joseph Okumu pia hakuweza kusafiri nchini kuwajibikia mechi hiyo baada ya kupata jeraha akisakatia timu yake.

Baada ya kuvaana na Misri, Stars itashiriki mechi yao ya mwisho ya kundi G ugenini dhidi ya Togo mnamo Machi 29.

You can share this post!

Matokeo mseto kwa mabondia wa Kenya jijini Kinshasa,...

Jinsi kamanda wa polisi Maragua alivyokataa Sh40,000 ambazo...