AFCON: Burkina Faso waingia robo-fainali baada ya kuzidi Gabon ujanja kupitia penalti

AFCON: Burkina Faso waingia robo-fainali baada ya kuzidi Gabon ujanja kupitia penalti

Na MASHIRIKA

BURKINA Faso walibandua Gabon kwenye raundi ya 16-bora ya Kombe la Afrika (AFCON) kupitia mikwaju ya penalti baada ya kuambulia sare ya 1-1 mwishoni mwa muda wa ziada mnamo Jumapili nchini Cameroon.

Ismahila Ouedraogo alifungia Burkina Faso penalti iliyowapa ushindi wa 7-6.

Gabon walikamilisha mechi na wachezaji 10 pekee uwanjani baada ya Sidney Obissa kuonyeshwa kadi nyekundu katika dakika ya 67. Hata hivyo, walisawazisha kupitia kwa Adama Guira mwishoni mwa kipindi cha pili. Awali, nahodha wa Burkina Faso, Bertrand Traore alikuwa amepoteza penalti kabla ya kuweka kikosi chake uongozini katika dakika ya 28.

Burkina Faso sasa watavaana na Tunisia katika hatua ya robo-fainali baada ya mabingwa hao wa 2004 kubandua Nigeria kwa kichapo cha 1-0.

Mechi iliyokutanisha Burkina Faso na Gabon uwanjani Limbe Omnisport ilikuwa yao ya kwanza tangu watoshane nguvu kwa sare ya 1-1 mnamo 2017.

Burkina Faso hawakuwa wamewahi kushinda Gabon katika mechi nne zilizopita tangu 2013. Walikamilisha kampeni za Kundi A katika nafasi ya pili kwa alama nne sawa na Cape Verde watakaoonana na Senegal mnamo Januari 24, 2022. Gabon waliokosa huduma za wachezaji wengi tegemeo kutokana na Covid-19, walishinda Comoros 1-0 kabla ya kusajili sare za 1-1 na 2-2 dhidi ya Ghana na Morocco mtawalia katika Kundi C.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Uingereza yadai Putin tayari kuivamia Ukraine

Vihiga Queens kileleni licha ya sare

T L