AFCON: Cameroon watandika Ethiopia na kufuzu kwa hatua ya 16-bora

AFCON: Cameroon watandika Ethiopia na kufuzu kwa hatua ya 16-bora

Na MASHIRIKA

WENYEJI Cameroon walikuwa wa kwanza kufuzu kwa hatua ya 16-bora ya Kombe la Afrika (AFCON) baada ya kutandika Ethiopia 4-1 katika mchuano wa pili wa Kundi A mnamo Alhamisi.

Mafowadi Vincent Aboubakar na Karl Toko-Ekambi walifunga mabao mawili kila mmoja baada ya Ethiopia waliotwaa ubingwa wa AFCON mnamo 1962 kuwekwa uongozini na Hotessa Dawa katika dakika ya nne.

Cameroon ambao ni mabingwa mara tano wa taji la AFCON, walitawazwa wafalme wa kipute hicho kwa mara ya mwisho mnamo 2017 nchini Gabon.

Walisawazishiwa na Toko-Ekambi katika dakika ya 12 kabla ya kuwekwa kifua mbele na Aboubakar katika dakika ya 53. Aboubakar anayechezea Al-Nassr ya Saudi Arabia, alifungia Cameroon bao la tatu katika dakika ya 55 kabla ya Toko-Ekambi wa Lyon kuzamisha kabisa chombo cha Ethiopia katika dakika ya 67.

Baada ya kufunga penalti mbili katika ushindi wa 2-1 dhidi ya Burkina Faso katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi A mnamo Januari 9, 2022, Aboubakar ambaye ni nahodha wa Cameroon sasa ndiye mfungaji bora wa kipute cha AFCON hadi kufikia sasa mwaka huu. Sasa anajivunia jumla ya mabao manne kutokana na mechi mbili.

Aidha, anajivunia rekodi ya mabao matano kutokana na mechi 10 za AFCON, hiyo ikimaanisha kwamba ameimarisha rekodi yake ya awali ya iliyokuwa ya bao moja kutokana na mechi nane ikiwemo ya fainali ya 2017 iliyomshuhudia akipachika wavuni goli la ushindi dhidi ya Misri ambao ni mabingwa mara saba wa AFCON.

Cameroon almaarufu The Indomitable Lions, wanafukuzia taji la sita la AFCON baada ya kushinda mechi sita mfululizo kwenye kivumbi hicho. Wameratibiwa kuchuana na Cape Verde katika mchuano wao wa mwisho wa Kundi A mnamo Januari 17, 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

CARABAO CUP: Arsenal walazimishia Liverpool sare tasa...

Viongozi wa Taita wazozana kuhusu ni nani bora machoni mwa...

T L