AFCON: Gambia na Mali pazuri kuingia hatua ya 16-bora baada ya kuambulia sare

AFCON: Gambia na Mali pazuri kuingia hatua ya 16-bora baada ya kuambulia sare

Na MASHIRIKA

GAMBIA na Mali waliweka hai matumaini ya kutinga hatua ya 16-bora ya Kombe la Afrika (AFCON) baada ya kusajili sare ya 1-1 mjini Limbe, Cameroon.

Mabao yote mawili katika mchuano huo wa Kundi F yalijazwa kimiani kupitia mikwaju ya penalti iliyothibitishwa kwa matumizi ya teknolojia ya VAR mwishoni mwa kipindi cha pili.

Ibrahima Kone alikuwa amewaweka Mali kifua mbele katika dakika ya 79 baada ya Ebou Adams kumwangusha Yves Bissouma ndani ya kijisanduku.

Musa Barrow alihakikisha kwamba Gambia wanaondoka ugani na alama moja baada ya kupachika wavuni mkwaju wa penalti baada ya Bissouma kunawa mpira.

Kufikia sasa, Gambia na Mali wanajivunia alama nne kila mmoja, matokeo ambayo yanatosha kuwakatia tiketi za kuingia hatua ya muondoano wakiwa miongoni mwa vikosi vitakavyoambulia nafasi za tatu makundi baada ya kusajili matokeo ya kuridhisha zaidi. Tunisia wanakamata nafasi ya tatu kwa pointi tatu huku Mauritania wakivuta mkia bila alama yoyote.

Gambia ambao wanaorodheshwa wa chini zaidi kimataifa miongoni mwa washiriki wote wa AFCON mwaka huu, walifungua kampeni zao kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Mauritania. Hii ni ya kwanza katika historia kwa Gambia wanaotiwa makali na kocha Tom Saintfiet kunogesha fainali za AFCON.

Ingawa Mali walitamalaki mchezo na kumiliki asilimia kubwa ya mpira, Gambia walivamia kwa kushtukiza huku Barrow akishuhudia kombora lake likibusu mwamba wa lango la Mali na kumwajibisha vilivyo kipa Ibrahim Mounkoro.

Bao la Mali lilikuwa la pili kwa Kone kufunga kwenye fainali za AFCON mwaka huu. Awali, nyota huyo alikuwa amefunga jingine katika ushindi wa 1-0 uliovunwa na Mali dhidi ya Tunisia katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi F.

Kone kwa sasa amefunga mabao 10 kutokana na mechi nane ndani ya jezi za Mali ambao tayari wamefuzu kwa mchujo wa kuwania mojawapo ya tiketi tano za kuwakilisha bara la Afrika kwenye fainali zijazo za Kombe la Dunia zitakazofanyika Qatar kati ya Novemba na Disemba 2022.

Gambia wameratibiwa kutandaza mchuano wao wa tatu na wa mwisho katika Kundi F mnamo Januari 20, 2022 huku Mali wakipimana ubabe na Mauritania.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

MAPISHI KIKWETU: Jinsi ya kuandaa masala ya nyama ya...

Liverpool warukia nafasi ya pili jedwalini baada ya kupiga...

T L