Michezo

AFCON: Ghana yatua kambini Abu Dhabi kwa mazoezi

June 5th, 2019 1 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

Wachezaji wote 29 wa kikosi cha Black Stars ya Ghana wamefika kambini Abu Dhabi kwa maandalizi makali kabla ya kuelekea Misri kushiriki fainali za Kombe la Mataifa Bingwa barani Afrika (Afcon).

Staa wa kikosi hicho, Jonathan Mensah alikuwa mchezaji wa mwisho kufika kwenye kambi hiyo inayoongozwa na kocha mkuu, Kwasi Appiah. Kadhalika, Ebenezer Ofori anayesakata soka nchini Amerika aliwasili leo Jumatano.

Ghana itashiriki katika mechi mbili za kirafiki kabla ya kuondoka kuelekea Misri kwa michuano hiyo ya bara. Jumapili, timu hiyo imepangiwa kupimana nguvu na Namibia kabla ya kuvaana na Msiri Jumatatu (Juni 10).

Katika fainali za Afcon, The Black Stars imepangwa kwenye Kundi F pamoja na mabingwa watetezi Cameroon, Benin na Guinea-Bissau, ambapo wataanza mechi zao Juni 25, katika uwanja wa Ismaili Sports Stadium.

Ghana ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa msimu huu baada ya kulikosa kwa kipindi cha miaka 30.