Michezo

AFCON: Kenya yatupwa katika chaka la simba

April 12th, 2019 2 min read

Na GEOFFREY ANENE

KENYA itatoana jasho na Senegal anayochezea Sadio Mane, Algeria na majirani Tanzania katika mechi za Kundi C za Kombe la Bara Afrika mwaka 2019 litakalofanyika Juni 21 hadi Julai 19 nchini Misri.

Droo ya mashindano haya ya mataifa manne imefanywa na mashujaa wa zamani Yaya Toure, El Hadji Diouf, Ahmed Hassan na Mustapha Hadji jijini Cairo mnamo Ijumaa.

Golikipa Patrick Matasi wa Harambee Stars afanya mazoezi katika picha hii ya Novemba 30, 2017, katika Utalii Sports Club. Picha/ Chris Omollo

Harambee Stars imewahi kukutana na Senegal mara tatu, yote katika Kombe la Afrika. Kenya ilitoka 0-0 mwaka 1990 kabla ya kulamibishwa sakafu 3-0 mwaka 1992 na kisha kulemewa 3-0 mwaka 2004 ambayo ndio mara ya mwisho Kenya ilishiriki AFCON.

Vijana wa kocha Sebastien Migne, ambao watajiandalia kombe hili nchini Ufaransa, wanafahamiana na Algeria. Wamekutana mara saba. Stars imechapwa mara tatu na pia kushinda tatu, huku mechi moja ikiishia sare. Mara ya mwisho mataifa haya yalikutana ni mwaka 1996 katika mechi za kufuzu kushiriki Kombe la Dunia ambapo Kenya ilipiga Algeria 3-1 jijini Nairobi Juni 2 nayo Algeria ikalipiza kisasi 1-0 nchini Algeria mnamo Juni 14.

Kenya na Tanzania zinajuana sana kwa sababu ya kushiriki mashindano ya Afrika Mashariki na Kati (Cecafa). Zimekutana mara 48. Kenya inajivunia kushinda Tanzania mara 20 ikiwemo mara ya mwisho zilikutana mwaka 2017, kuchapwa mara 14, huku mechi 14 zikitamatika bila mshindi.

Katika mechi za kufuzu kushiriki mashindano haya ya mataifa 24, Kenya ilimaliza ya pili katika Kundi F nyuma ya Ghana baada ya kupoteza mechi yake ya mwisho 1-0 jijini Accra mnamo Machi 23, 2019.

Ilikuwa imefuzu baada ya kuchapa Ghana 1-0 jijini Nairobi mwezi Septemba na kukaba Ethiopia 0-0 nchini Ethiopia kabla ya kuibwaga 3-0 jijini Nairobi mwezi Oktoba mwaka 2018. Senegal na Algeria zilifuzu mapema, huku Tanzania ikihitajika kuchapa majirani Uganda 3-0 katika mechi ya mwisho kurejea AFCON baada ya kuwa nje tangu mwaka 1980.

Baadhi ya majina makubwa katika timu za kundi C ni nahodha wa Kenya kiungo Victor Wanyama anayechezea Tottenham Hotspur nchini Uingereza, mshambuliaji wa Liverpool Mane na Mbwana Samatta wa Tanzania.

Kwa mara ya kwanza katika historia ya AFCON, ambayo mwaka huu itakuwa makala ya 32, eneo la Cecafa litawakilishwa na mataifa manne. Mbali na Kenua, Uganda na Tanzania, Burundi pia ilifuzu. Ni mara ya kwanza kabisa Burundi kufuzu kushiriki mashindano haya ya kifahari.

Misri, ambao walifuzu moja kwa moja kama wenyeji, ingawa pia walikuwa wameshajikatia tiketi katika mechi za mchujo kabla ya kutwikwa majukumu ya uenyeji baada ya Cameroon kupokonywa maandalizi kwa kukosa kuwa tayari kwa muda ufaao.

Mabingwa watetezi ni Cameroon, ambao walijikatia tiketi baada ya kulemea Comoros katika mechi ya mwisho mwezi uliopita. Mauritania na Madagascar pia zinashiriki mashindano haya kwa mara ya kwanza kabisa.

MAKUNDI YA AFCON 2019:

Kundi A – Misri, DR Congo, Uganda, Zimbabwe;

Kundi B – Nigeria, Guinea, Madagascar, Burundi;

Kundi C – Senegal, Algeria, Kenya, Tanzania;

Kundi D – Morocco, Ivory Coast, Afrika Kusini, Namibia;

Kundi E – Tunisia, Mali, Mauritania, Angola;

Kundi F – Cameroon, Ghana, Benin, Guinea-Bissau.