Michezo

AFCON: Kundi F la Kenya sasa li wazi

September 10th, 2018 1 min read

Na Geoffrey Anene

KUNDI ‘F’ la mchujo wa kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) mwaka 2019 limetupwa wazi baada ya Ethiopia kufuata nyayo za Kenya kwa kuadhibu Sierra Leone 1-0 mjini Awassa hapo Septemba 9, 2018.

Harambee Stars ya Kenya ilicharaza Black Stars ya Ghana 1-0 uwanjani Kasarani jijini Nairobi mnamo Septemba 8.

Kenya na Ethiopia zilianza kampeni zao kwa kupigwa katika nchi hizo za Magharibi mwa Afrika mwezi Juni mwaka 2017.

Wakenya walizabwa 2-1 na Sierra Leone jijini Freetown kabla ya kufufua matumaini yao kwa kushangaza Ghana, ambayo ilikuwa imepigiwa upatu kutamba kutokana na rekodi yake nzuri dhidi ya Kenya pamoja na kuwa na kikosi kizoefu na pia kuorodheshwa nafasi 67 juu ya nambari 112 Kenya kwenye viwango bora vya Shirikisho la Soka Duniani (FIFA). Sierra Leone inashikilia nafasi ya 111 duniani nayo Ethiopia iko katika nafasi ya 151.

Baada ya mataifa haya kusakata mechi zao za pili, Ghana inasalia kileleni kwa alama tatu sawa na nambari mbili Kenya, ambayo imeruka Sierra Leone. Sierra Leone na Ethiopia zinashikilia nafasi mbili za mwisho pia kwa alama tatu kila mmoja.

Timu hizi nne zitaingia mechi za raundi ya tatu na nne mwezi Oktoba zikiwa na nafasi nzuri ya kuruka juu ya jedwali. Kenya itazuru Ethiopia na kisha kualika majirani hawa jijini Nairobi nayo Ghana itakaribisha Sierra Leone kabla ya kusafiri jijini Freetown.

Kenya itaalika Sierra Leone jijini Nairobi mwezi Novemba mwaka 2018 kabla ya kukamilisha kampeni yake ya kutafuta kurejea AFCON tangu mwaka 2004 dhidi ya Ghana kwao mwezi Machi mwaka 2019. Timu mbili za kwanza zitaingia makala yajayo ya AFCON.