HabariMichezo

AFCON: Lazima kieleweke Cairo!

June 21st, 2019 2 min read

Na JOHN ASHIHUNDU

KIKOSI cha Harambee Stars ni miongoni mwa timu 24 zitakazoshiriki katika fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika (AFCON), ambazo kwa mara ya kwanza, Afrika Mashariki itawakilishwa na mataifa manne kwa mpigo.

Kenya, Uganda, Tanzania na Burundi zote zimefuzu kwa fainali hizo zitakazoanza Ijumaa hii hadi Julai 19 Cairo, Misri.

Mechi ya ufunguzi itakuwa ya Kundi kati ya wenyeji, Misri dhidi ya Zimbabwe kabla ya Uganda na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) kuingia kwenye mechi ya pili ya kundi hilo.

Uganda wameendelea kushikilia kiwango bora kwa timu ya ukanda huu, lakini watakuwa mbele ya DRC ambao wanauzoefu mkubwa katika mechi za kimataifa, baada ya kushiriki michuano hiyo mara kwa mara.

Harambee Stars ambayo imefuzu baada ya kusubiri kwa kipindi cha miaka 15, imepangiwa kwenye kundi moja na Taifa Stars ya Tanzania ambayo imerejea baada ya miaka 39.

Timu nyingine kwenye Kundi hilo la C ni Senegal ya mfumania nyavu matata, Sadio Mane wa Liverpool pamoja na vigogo wa Algeria wanaojivunia majina makubwa akiwemo Riyad Mahrez anayesakatia klabu ya Manchester City ya ligi kuu ya Uingereza (EPL).

Kenya na Tanzania zitaanza mechi zao Jumapili katika uwanja wa june 30 jijini Cairo. Harambee Stars chini ya kocha Sebastien Migne itaaanza kampeni dhidi ya Algeria, siku ambayo Tanzania imepangiwa kuvaana na Senegal ambayo itakuwa bila staa Mane.

Mshambuliaji huyo matata aliye pia nahodha wa kikosi hicho cha Lions of Teranga amefungiwa mechi moja baada ya kuonyeshwa kadi mbili za njano katika mechi za kufuzu dhidi ya Equatoria Guinea na Madagascar ambazo walishinda 1-0 na 2-0 mtawaliwa.

Katika mechi za Ijumaa, Uganda Cranes wataongozwa na kipa matata, Denis Onyango klabu ya Mamelodi Sundowns nchini Afrika Kusini ambaye anaamini wanaweza kuibwaga DRC ambaye imewahi kushiriki fainali ya Kombe la Dunia na pia mabingwa wa AFCON mnamo 1968 na 1974.

Kikosi hicho chini ya kocha Sebastien Desabre vile vile kina nyota kadhaa wanaosakata soka katika mataifa ya kigeni, mbali na wale wanaochezea klabu za nyumbani kwenye ligi kuu ya UPL, nchini Uganda.

Uganda ilibanduliwa katika hatua ya kwanza wakati wa AFCON za 2017, wakati DRC wakitinga robo-fainali na kutolewa na Ghana kwa 2-1.

Hapo awali, mnamo 2015, DRC ilimaliza michuano hiyo katika nafasi ya tatu, kama walivyofanya pia mwaka wa 1998.

DRC ambayo ni miongoni mwa timu zinazopewa nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa wa mwaka huu, ilitwaa taji hilo kwa mara ya mwisho mnamo 1974, fainali hizo zilipofanyika nchini Misri, na ikiwa hitoria itajirudia, basi huenda ikawa wakati wao kulibeba tena.