AFCON: Limbukeni Sierra Leone waridhika kutoka sare na mabingwa watetezi Algeria

AFCON: Limbukeni Sierra Leone waridhika kutoka sare na mabingwa watetezi Algeria

Na MASHIRIKA

ALGERIA walianza kutetea ubingwa wa Kombe la Afrika (AFCON) nchini Cameroon kwa sare tasa dhidi ya Sierra Leone katika mchuano wa Kundi E linalojumuisha pia Equatorial Guinea na mabingwa wa 2015, Ivory Coast.

Sierra Leone walianza kipindi cha kwanza kwa matao ya juu huku Alhaji Kamara akipoteza nafasi mbili za wazi.

Fowadi Yacine Brahimi wa Algeria naye alishindwa kumwacha hoi kipa Mohamed Nbalie Kamara wa Sierra Leone licha ya kusalia naye uso kwa macho huku kombora la nahodha Riyad Mahrez wa Algeria likibusu mwamba wa goli.

Nbalie Kamara alifanya kazi ya ziada mwishoni mwa kipindi cha pili na kunyima Ramy Bensebaini na Baghdad Bounedjah nafasi mbili za kuweka Algeria kifua mbele.

Steven Caulker ambaye ni beki wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza alijituma vilivyo na akazuia makombora mawili muhimu na kuokoa chombo cha Sierra Leone wanaogesha kipute cha AFCON kwa mara ya kwanza tangu 1996. Caulker alihamia Sierra Leone mwaka mmoja uliopita baada ya kupata uraia wa taifa hilo.

Sare hiyo ilishuhudia Algeria wakiendeleza rekodi ya kutoshindwa katika mechi 35 mfululizo za kimataifa na hivyo kukaribia rekodi ya Italia waliowahi kutandaza jumla ya michuano 37 bila kupoteza.

Hata hivyo, kocha Djamel Belmadi hakuridhishwa na matokeo ya kikosi chake kinachoorodheshwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) katika nafasi ya 31 ikizingatiwa kwamba Sierra Leone wanashikilia nafasi ya 108 duniani.

Sierra Leone kwa sasa wanajiandaa kumenyana na Ivory Coasy mnamo Januari 16, 2022 huku Algeria wakimenyana na Equatorial Guinea siku hiyo.

Hii ni mara yake ya pili kwa kocha John Keister kudhibiti mikoba ya timu ya taifa ya Sierra Leone. Aliwahi kuchezea vikosi mbalimbali nchini Uingereza, zikiwemo klabu za Walsall na Margate na akawajibikia Sierra Leone kati ya 1997 na 2003.

Mbali na Caulker, kikosi cha Sierra Leone kinajumuisha pia mvamizi wa zamani wa Middlesbrough nchini Uingereza, Kei Kamara, 37. Algeria walitawazwa wafalme wa AFCON mnamo 2019 baada ya kupepeta Senegal 1-0 nchini Misri.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Beki wa timu ya taifa ya Uturuki afariki dunia akiwa na...

Maseneta kuendesha vikao vya kukusanya maoni kuhusu mswada...

T L