Michezo

AFCON: Macho kwa Ighalo leo Nigeria na Tunisia zikipigania shaba

July 17th, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

CAIRO, MISRI

TUNISIA na Nigeria walibanduliwa kwenye fainali za AFCON mwaka 2019 mwishoni mwa wiki jana nchini Misri.

Hii ni baada ya timu hizo kuzidiwa maarifa na Senegal na Algeria mtawalia.

Kudenguliwa kwao katika hatua ya nusu-fainali kuliwaweka katika ulazima wa kuvaana leo ugani Al Salam, Cairo katika mechi ya kutafuta mshindi nambari tatu na nne mtawalia.

Nigeria wanajivunia kusajili ushindi wa AFCON mnamo 1980, 1994 na 2013 huku Tunisia wakitawazwa mabingwa mnamo 2004 mbele ya mashabiki wao wa nyumbani.

Chini ya kocha Gernot Rohr, Super Eagles wa Nigeria wanapigiwa upatu wa kuzamisha chombo cha wapinzani wao Carthage Eagles hasa ikizingatiwa kiwango cha kusuasua kwao katika michuano ya hatua ya makundi.

Baada ya kuanza vibaya kivumbi hiki, Tunisia walianza kujinyanyua katika hatua ya 16-bora, japo utata mwingi ulitawala ushindi waliousajili dhidi ya Black Stars ya Ghana katika awamu hiyo ya mwondoano.

Ufanisi wa kuwabandua Ghana kupitia mikwaju ya penalti uliwapa hamasa zaidi ya kuwachabanga limbukeni Madagascar 3-0 katika robo-fainali, na hivyo kujikatia tiketi ya kuchuana na Senegal ambao hii ni fainali yao ya pili kushiriki tangu 2002.

Kosa la kipa Mouez Hassan mwishoni mwa muda wa ziada liliwapa Tunisia nafasi ya kujifunga na hivyo kubanduliwa na Senegal.

Awali, vikosi vyote viwili vilipoteza mikwaju ya penalti huku kilio cha Tunisia kupokezwa mkwaju mwingine wa penalti mwishoni mwa kipindi cha pili kikipuuzwa na refa baada ya kushauriana na wataalamu wa teknolojia ya video ya VAR.

Kwa mujibu wa kocha Alain Giresse wa Tunisia, refa alistahili kuwapa penalti kwa kuwa Idrissa Gueye alionekana kuunawa mpira aliopokezwa kwa kichwa na mwenzake Salif Sane ndani ya kisanduku.

Wakiwa miongoni mwa timu zilizopigiwa upatu wa kunyanyua ubingwa wa mwaka huu, Nigeria walifaulu kuwabandua mabingwa watetezi Cameroon katika hatua ya 16-bora kwa mabao 3-2 kabla ya kuwazima Afrika Kusini kwa magoli 2-1 katika robo-fainali.

Katika nusu-fainali, Algeria waliwekwa kifua mbele kupitia bao la beki wa Udinese, William Troost-Ekong aliyejifunga kwa kujaza kimiani krosi ya nyota matata wa Manchester City, Riyad Mahrez.

Mahrez azima ndoto ya Super Eagles

Ingawa Odion Ighalo aliwarejesha Nigeria mchezoni baada ya kuwafungia penalti, Algeria walikizamisha chombo cha wapinzani wao kupitia ikabu iliyochanjwa na Mahrez mwishoni mwa kipindi cha pili.

“Ilitulazimu kusubiri hadi dakika za mwisho ili kusajili ushindi dhidi ya Afrika Kusini katika robo-fainali. Algeria nao wametutoa kwenye nusu-fainali sekunde chache kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa kipindi cha pili kupulizwa. Huo ndio mchezo wa soka ambao kwa kweli, hauna adabu,” akasema Rohr.

Ighalo ambaye kwa sasa anaongoza orodha ya wafungaji bora kwa mabao manne, anatarajiwa kuwatambisha zaidi Nigeria kadri wanavyopania kutia kapuni nishani ya shaba.

Nigeria ambayo inajivunia wachezaji nyota kama vile Ighalo, Alex Iwobi na Ahmed Musa, watakuwa wakitafuta kudumisha rekodi ya kutoshindwa na Tunisia hadi mechi nne.