Michezo

Afcon: Morocco wafungishwa virago na Afrika Kusini

January 31st, 2024 2 min read

Na MASHIRIKA

ABIDJAN, COTE D’IVOIRE

MASHABIKI wa soka waliendelea kushuhudia matokeo ya kustaajabisha baada ya Morocco kubanduliwa na Afrika Kusini iliyoshinda 2-0 Jumanne usiku na kufuzu kwa robo-fainali za Kombe la Taifa Bingwa Afrika (Afcon 2023).

Mali pia ilitinga hatua hiyo baada ya kuzima Burkina Faso 2-1 katika mechi nyingine iliyochezewa Amadou Gon Coulibaly mjini Korhogo.

Ni matokeo ya Morocco kuvungishwa virago mapema katika mechi iliyochezewa ugani Laurent Pokou yaliyowaacha wengi katika mshangao hasa baada ya staa wa Morocco Achraf Hakimi kupoteza penalti dakika ya 85 ambayo ingesawazisha mambo, huku kiungo Sofyan Amrabat wa Manchester United akitolewa kwa kadi nyekundu mechi hiyo ikielekeza kumalizika.

Penaltii hiyo ilipeanwa baada ya Mothobi Mvala kuunawa mpira katika eneo la hatari kufuatia kombora la Ayoub El Kaabi.

Afrika Kusini ambayo itakutana na Cape Verde alipata mabao hayo ya ushindi dakika za 57 na 95 kupitia kwa mshambuliaji Evidence Makgopa anayechezea klabu ya Orlando Pirates na kiungo mahiri Teboho Mokoena wa Mamelodi Sundowns.

Morocco wanaoorodheshwa katika nafasi ya 13 Duniani baada mnamo 2022 kutinga nusu-fainali ya Kombe la Dunia nchini Qatar waliwekewa nafasi kubwa ya kushinda mechi hiyo, lakini mashabiki wao hawakuamini macho yao waliposhuhudia wakibanduliwa mapema.

Huku wakiorodheshwa katika nafasi ya 66, Afrika Kusini waliotwaa ubingwa michuano hii 1996 watatakiwa kujitahidi zaidi dhidi ya Cape Verde, Jumamosi baada ya kubanduliwa katika robo-fainali fainali hizo zilipofanyika nchini Misri mnamo 2019. Cape Verde wanakamata nafasi ya 73 Duniani.

Morocco ambayo ndiyo inayoorodheshwa katika nafasi ya kwanza barani Afrika, itasubiri hadi 2025 watakapokuwa waandalizi wa michuano hiyo kumaliza kiu yao ya kungojea tangu waibuke washindi 1976.

Wachanganuzi wengi wa spoti wamehusisha kuondolewa kwao mapema na majeraha kwa wachezaji kadhaa tegemeo akiwemo Hakim Ziyech aliyeumia wakicheza na Zambia, pamoja na kukosekana kwa staa Sofiane Boufal.

Katika mechi iliyochezewa Amadou Gon Coulibaly mjini Korhogo, Mali walifuzu kwa robo-fainali na sasa watakutana na wenyeji Cote d’ Ivoire (Ivory Coast) waliofuzu hapo awali baada ya kutandika mabingwa watetezi, Senegal kupitia mikwaju ya penalti.

Mali wanaorodheshwa katika nafasi ya 51 Duniani wakati Cote d’Ivoire wakipangwa katika nafasi ya 49 katika viwango hivyo vya Shirikisho la Kimataifa la Soka (FIFA).

Katika robo-fainali ya Ijumaa ugani Felix Houphouet-Boigny, Nigeria wanaoshikilia nafasi ya 42 Duniani watakabiliana na Angola wanaoshikilia nafasi ya 117.

Siku hiyo hiyo, DR Congo inayotosheka na nafasi ya 67 Duniani itakutana na Guinea–katika nafasi ya 80–ugani Stade Olympique Allassane Quattara.

Mechi za Jumamosi ni Mali na Cote d’Ivoire (Stade de Bouake), na Cape Verde dhidi ya Afrika Kusini (Stade Charles Konan Banny de Yamoussoukro).

Uchambuzi zaidi na John Ashihundu