AFCON: Nigeria yanyoa Sudan katika Kundi D na kuingia 16-bora

AFCON: Nigeria yanyoa Sudan katika Kundi D na kuingia 16-bora

Na MASHIRIKA

NIGERIA walitinga hatua ya 16-bora ya Kombe la Afrika (AFCON) baada ya kukung’uta Sudan 3-1 mnamo Jumamosi nchini Cameroon.

Samuel Chukwueze alifunga bao la kwanza la Super Eagles ya Nigeria iliyopata mabao mawili zaidi kupitia kwa Taiwo Awoniyi na Moses Simon katika dakika za 45 na 46 mtawalia.

Walieldin Khedr alijaza kimiani bao la Sudan kupitia penalti katika dakika ya 70 baada ya Ola Aina kuchezea Mustafa Karshoum visivyo ndani ya kijisanduku.

Nigeria walishinda mechi yao ya kwanza ya Kundi D dhidi ya Misri kwa 1-0. Ushindi huo uliwapa motisha ya kuteremkia Sudan inayoshikilia nafasi ya 125 duniani kwa matao ya juu zaidi.

Nigeria kwa sasa wanatiwa makali na kocha mshikilizi Augustine Eguavoen aliyepokezwa mikoba baada ya Shirikisho la Soka la nchi hiyo (NFF) kumtema mkufunzi Gernot Rohr wiki nne kabla ya kipenga cha kuashiria mwanzo wa AFCON kupulizwa.

Nigeria wanaofukuzia ubingwa wa AFCON kwa mara ya nne, watakamilisha kampeni zao za Kundi D dhidi ya Guinea-Bissau mnamo Januari 19, 2022 huku Guinea-Bissau wakimenyana na wafalme mara saba, Misri.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Aston Villa watoka nyuma na kulazimishia Man-Utd sare ya...

NYOTA WA WIKI: Antonio Rudiger

T L